Jumanne. 23 Aprili. 2024

Masomo ya Misa

Jumatatu ya 1 ya Majilio (Jumatatu, Novemba 28, 2022)  

Somo la 1

Isa 2:1-5

Hili ni neno aliloliona Isaya mwana wa Amozi katika habari za Yuda na Yerusalemu. Na itakuwa katika siku za mwisho, mlima wa nyumba ya Bwana utawekwa imara juu ya milima, nao utainuliwa juu ya vilima; na mataifa yote watauendea makundi makundi. Na mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu mlimani mwa Bwana, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake; maana katika Sayuni itatoka sheria na neno la Bwana katika Yerusalemu. Naye atafanya hukumu katika mataifa mengi, atawakemea watu wa kabila nyingi; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa linguine, wala hawatajifunza vita tena kamwe. Enyi wa nyumba ya Israeli, njoni, twende katika nuru ya Bwana.

Wimbo wa Katikati

Zab 122:1-4, 8, 9

Nalifurahi waliponiambia,
Na twende nyumbani kwa Bwana.
Miguu yetu imesimama
Ndnai ya malango yako, Ee Yerusalemu. 
(K) Nalifurahi waliponiambia, na twende nyumbani kwa Bwana.

Ee Yerusalemu uliyejengwa
Kama mji ulioshikamana,
Huko ndiko walikopanda kabila,
Kabila za Bwana. 
(K) Nalifurahi waliponiambia, na twende nyumbani kwa Bwana.

Kwa ajili ya ndugu zangu na rafiki zangu
Niseme sasa, Amani ikae nawe.
Kwa ajili ya nyumba ya Bwana, Mungu wetu,
Nikutafutie mema. 
(K) Nalifurahi waliponiambia, na twende nyumbani kwa Bwana.

Shangilio

Zab 80:4

Aleluya, aleluya,
Ee Bwana, Mungu wa majeshi, hata lini? Utayaghadhibikia maombi ya watu wako?
Aleluya.

Injili

Mt 8:5-11

Hata alipoingia Kapernaumu, akida mmoja alimjia, akamsihi, akisema, Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani, mgonjwa wa kupooza, anaumwa sana. Yesu akamwambia, Nitakuja, nimponye. Yule akida akamjibu, akasema, Bwana, mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu, lakini sema neno tu, na mtumishi wangu atapona. Kwa maana nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya. Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia waliomfuata, Amin, nawaambieni, Sijaona imani kubwa namna hii, yeyote katika Israeli. Nami nawaambieni, kwamba, wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi na wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni.

Maoni


Ingia utoe maoni