Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumanne ya 34 ya Mwaka (Jumanne, Novemba 22, 2022)  

Somo la 1

Ufu 14:14–19

Mimi, Yohane, niliona, na tazama, wingu jeupe, na juu ya wingu hilo ameketi mmoja, mfano wa Mwanadamu, mwenye taji ya dhahabu juu ya kichwa chake, na katika mkono wake mundu mkali. Na malaika mwingine akatoka katika hekalu, akimlilia kwa sauti kuu yeye aliyekuwa ameketi juu ya lile wingu, Tia mundu wako, ukavune; kwa kuwa saa ya kuvuna imekuja; kwa kuwa mavuno ya nchi yamekomaa. Na yeye aliyeketi juu ya wingu akautupa mundu wake juu ya nchi, nchi ikavunwa. Kisha malaika mwingine akatoka katika lile hekalu lililoko mbinguni, yeye naye ana mundu mkali. Na malaika mwingine akatoka katika ile madhabahu, yule mwenye mamlaka juu ya moto; naye akamlilia kwa sauti kuu yule mwenye mundu ule mkali, akisema, Tia mundu wako mkali, ukachume vichala vya mzabibu wa nchi, maana zabibu zake zimeiva sansa. Malaika yule akautupa mundu wake hata nchi, akauchuma mzabibu wa nchi, akazitupa zabibu katika shinikizo hilo kubwa la ghadhabu ya Mungu.

Wimbo wa Katikati

Zab 96:10–13

Semeni katika mataifa, Bwana ametamalaki;
Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike,
Atawahukumu watu kwa adili.
Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie,
Bahari na ivume na vyote viijazavyo.
(K) Bwana atauhukumu ulimwengu kwa haki.

Mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo,
Ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha;
Mbele za Bwana, kwa maana anakuja,
Kwa maana anakuja aihukumu nchi.
Atauhukumu ulimwengu kwa haki,
Na mataifa kwa uaminifu wake.
(K) Bwana atauhukumu ulimwengu kwa haki.

Shangilio

Yak 1:21

Aleluya, aleluya,
Pokeeni kwa upole neno la Mungu, lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zenu.
Aleluya.

Injili

Lk 21:5-11

Watu wa kadha wa kadha walipokuwa wakiongea habari za hekalu, jinsi lilivyopambwa kwa mawe mazuri na sadaka za watu, Yesu alisema, Haya mnayoyatazama, siku zitakuja ambapo halitasalia jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa. Wakamwuliza wakisema, Mwalimu, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini ishara ya kuwa mambo hayo ya karibu kutukia? Akasema, Angalieni, msije mkadanganyika, kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ndiye; tena, Majira yamekaribia. Basi msiwafuate hao. Nanyi mtakaposikia habari za vita na fitina, msitishwe; maana, hayo hayana budi kutukia kwanza, lakini ule mwisho hauji upesi. Kisha aliwaambia, Taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na matetemeko makubwa ya nchi; na njaa na tauni mahali mahali; na mambo ya kutisha na ishara kuu kutoka mbinguni.

Maoni


Ingia utoe maoni