Masomo ya Misa
Jumatatu ya 31 ya Mwaka (Jumatatu, Oktoba 31, 2022)
Fil 2:1-4
Ikiwako faraja yo yote katika Kristo, yakiwako matulizo yo yote ya mapenzi, ukiwako ushirika wo wote wa Roho, ikiwako huruma yo yote na rehema, ijalizeni furaha yangu, ili mwe na nia moja, wenye mapenzi mamoja, wenye roho moja, mkinia mamoja. Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.
Zab 131
Bwana, moyo wangu hauna kiburi,
Wala macho yangu hayainuki.
Wala sijishughulishi na mambo makuu,
Wala na mambo yashindayo nguvu zangu.
(K) Moyo wangu uwe na amani kwako, Ee Bwana
Hakika nimeituliza nafsi yangu, Na kuinyamazisha.
Kama mtoto aliyeachishwa Kifuani mwa mama yake;
Kama mtoto aliyeachishwa,
Ndivyo roho yangu ilivyo kwangu.
(K) Moyo wangu uwe na amani kwako, Ee Bwana
Ee Israeli, umtarajie Bwana, Tangu leo na hata milele.
(K) Moyo wangu uwe na amani kwako, Ee Bwana
Zab. 130:5
Aleluya, aleluya,
Roho yangu inamngoja Bwana, na neno lake nimelitumainia.
Aleluya.
Lk 14:12-14
Yesu alimwambia na yule aliyemwalika, Ufanyapo chakula cha mchana au cha jioni, usiwaite rafiki zako, wala ndugu zako, wala jamaa zako, wala jirani zako wenye mali; wao wasije wakakualika wewe ukapata malipo. Bali ufanyapo karamu waite maskini, vilema, viwete, vipofu, nawe utakuwa heri, kwa kuwa hao hawana cha kukulipa; kwa maana utalipwa katika ufufuo wa wenye haki.
Maoni
Ingia utoe maoni