Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumanne ya 29 ya Mwaka (Jumanne, Oktoba 18, 2022)  

Somo la 1

Efe 2:12–22

Msisahau kwamba zamani zile mlikuwa hamna Kristo, mmefarakana na jamii ya Israeli, wageni wasio wa maagano ya ahadi ile. Mlikuwa hamna tumaini, hamna Mungu duniani. Lakini sasa, katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo. Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja; akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga. Naye akiisha kuuondoa ule uadui kwa mwili wake; ndiyo sheria ya amri zilizo katika maagizo; ili afanye hao wawili kuwa mtu mpya mmoja ndani ya nafsi yake; akafanya amani. Akawapatanisha wote wawili na Mungu katika mwili mmoja, kwa njia ya msalaba, akiisha kuufisha ule uadui kwa huo msalaba. Akaja akahubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali, na amani kwao wale waliokuwa karibu. Kwa maana kwa yeye sisi sote tumepata njia ya kumkaribia Baba katika Roho mmoja. Basi tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu. Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe na jiwe kuu la pembeni. Katika yeye jingo lote linaungamanishwa vema na kuku ahata liwe hekalu takatifu katika Bwana. Katika ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho.

Wimbo wa Katikati

Zab 85:9–14

Nisikie atakavyosema Bwana,
Maana atawaambia watu wake amani.
Hakika wokovu wake u karibu na wamchao,
Utukufu ukae katika nchi yetu.
(K) Bwana anawaambia watu wake amani.

Fadhili na kweli zimekutana,
Haki na amani zimebusiana.
Kweli imechipuka katika nchi,
Haki imechungulia kutoka mbinguni.
(K) Bwana anawaambia watu wake amani.

Bwana atatoa kilicho chema,
Na nchi yetu itatoa mazao yake.
Haki itakwenda mbele zake,
Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia.
(K) Bwana anawaambia watu wake amani.

Shangilio

Yn 10:27

Aleluya, aleluya,
Kondoo wangu waisikia sauti yangu, nami nawajua, nao wanifuata.
Aleluya.

Injili

Lk 12:35-38

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka; nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara. Heri watumwa wale, ambao bwana wao ajapo atawakuta wanakesha. Amin, nawaambieni, atajifunga na kuwakaribisha chakulani, atakuja na kuwahudumia. Na akija zamu ya pili, au akija zamu ya tatu, na kuwakuta hivi, heri watumwa hao.

Maoni


Ingia utoe maoni