Masomo ya Misa
Alhamisi ya 28 ya MWaka (Alhamisi, Oktoba 13, 2022)
Efe 1:1, 3–10
Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu; kwa watakatifu wanaomwamini Kristo Yesu. Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa Baraka zote za rohoni, katika ulimwengu war oho, ndani yake Kristo; kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo. Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na Uradhi wa mapenzi yake. Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa. Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake. Naye alituzidishia hiyo katika hekima yote na ujuzi; akiisha kutujulisha siri ya mapenzi yake, sawasawa na Uradhi wake, alioukusudia katika yeye huyo. Yaani, kuleta madaraka ya wakati mkamilifu atavijumlisha vitu vyote katika Kristo, vitu vya mbinguni na vitu vya duniani pia.
Zab 98:1–6
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu,
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.
(K) Bwana ameufunua wokovu wake.
Bwana ameufunua wokovu wake,
Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli.
(K) Bwana ameufunua wokovu wake.
Miisho yote ya dunia imeuona
Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi.
(K) Bwana ameufunua wokovu wake.
Mwimbieni Bwana zaburi kwa kinubi,
Kwa kinubi na sauti ya zaburi.
Kwa panda na sauti ya baragumu,
Shangilieni mbele za Mfalme, Bwana.
(K) Bwana ameufunua wokovu wake.
Zab 119:105
Aleluya, aleluya,
Neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu.
Aleluya.
Lk 11:47-54
Yesu aliwaambia wanasheria: Ole wenu, kwa kuwa mwajenga maziara ya manabii, na baba zenu ndio waliowaua. Basi, mwashuhudia na kuziridhia kazi za baba zenu; kwa kuwa wao waliwaua nanyi mwawajengea maziara. Na kwa sababu hiyo hekima ya Mungu ilisema, Tazama, nitatuma kwao manabii na mitume, nao watawaua baadhi yao na kuwafukuza, ili kwa kizazi hiki itakwe damu ya manabii wote, iliyomwagika tangu kupigwa msingi wa ulimwengu; tangu damu ya Habili hata damu ya Zakaria, aliyeuawa kati ya madhabahu na hekalu. Naam, nawaambieni ya kwamba itatakwa kwa kizazi hiki. Ole wenu, enyi wanasheria, kwa kuwa mmeuondoa ufunguo wa maarifa; wenyewe hamkuingia na wale waliokuwa wakiingia mmewazuia. Alipotoka humo, waandishi na Mafarisayo walianza kumsonga vibaya, na kumchokoza kwa maswali mengi, wakimvizia, ili wapate neno litokalo kinywani mwake.
Maoni
Ingia utoe maoni