Masomo ya Misa
Jumamosi ya 27 ya Mwaka (Jumamosi, Oktoba 08, 2022)
Gal 3:22–29
Andiko limeyafunga yote chini ya nguvu ya dhambi, makusudi hao waaminio wapewe ile ahadi kwa Imani ya Yesu Kristo. Lakini kabla ya kuja ile Imani tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ije ile Imani itakayofunuliwa. Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa Imani. Lakini, iwapo Imani imekuja, hatupo tena chini ya kiongozi. Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya Imani katika Kristo Yesu. Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu. Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi.
Zab 105:2–7
Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi,
Zitafakarini ajabu zake zote.
Jisifuni kwa jina lake takatifu,
Na ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana.
(K) Bwana analikumbuka agano lake milele.
Mtakeni Bwana na nguvu zake,
Utafuteni uso wake sikuzote.
Zikumbukeni ajabu zake alizozifanya,
Miujiza yake na hukumu za kinywa chake.
(K) Bwana analikumbuka agano lake milele.
Enyi wazao wa Ibrahimu, mtumishi wake,
Enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
Yeye, Bwana, ndiye Mungu wetu;
Duniani mwote mna hukumu zake.
(K) Bwana analikumbuka agano lake milele.
Zab 119:18
Aleluya, aleluya,
Unifumbue macho yangu niyatazame maajabu yatokayo katika sheria yako.
Aleluya.
Lk 11:27-28
Ikawa, Yesu alipokuwa akisema, mwanamke mmoja katika mkutano alipaza sauti yake, akamwambia Heri tumbo lililokuzaa, na matiti uliyonyonya. Lakini yeye alisema, Afadhali, heri walisikiao neno la Mungu na kulishika.
Maoni
Ingia utoe maoni