Jumanne. 23 Aprili. 2024

Masomo ya Misa

Sikukuu ya Malaika Wakuu Gabriel, Mikaeli na Rafae (Alhamisi, Septemba 29, 2022)  

Somo la 1

Dan 7:9-10,13-14

Nilitazama viti vya enzi vikawekwa, na mmoja aliye mzee wa siku ameketi; mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji, na nywele za kichwa chake kama sufu safi; kiti chake cha enzi kilikuwa miali ya moto, na gurudumu zake moto uwakao. Mto kama wa moto ukatoka ukapita mbele zake, maelfu elfu wakamtumikia, na elfu kumi wakasimama mbele zake; hukumu ikawekwa, na vitabu vikafunuliwa. Nikaona katika njozi za usiku, na tazama mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo mzee wa siku, wakamleta karibu naye. Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele ambayo haitapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa.

Wimbo wa Katikati

Zab 138:1-5

Nitakushukuru kwa moyo wangu wote,
Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.
Nitasujudu nikilikabili hekalu lako takatifu.
(K) Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.

Kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako,
Kwa maana umeikuza ahadi yako,
Kuliko jina lako lote.
Siku ile niliyokuita uliniitikia,
Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu.
(K) Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.

Ee Bwana, wafalme wote wa dunia watakushukuru,
Watakapoyasikia maneno ya kinywa chako.
Naam, wataziimba njia za Bwana,
Kwa maana utukufu wa Bwana ni mkuu
(K) Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.

Shangilio

Zab 105:3

Aleluya, aleluya,
Mhimidini Bwana, enyi majeshi yake yote, ninyi watumishi wake mfanyao mapenzi yake.
Aleluya.

Injili

Yn 1:47-51

Yesu alipomwona Nathanaeli anakuja kwake akanena habari zake, Tazama, Mwisraeli kweli kweli, hamna hila ndani yake. Nathanaeli akamwambia, Umepataje kunitambua? Yesu akajibu, akamwambia, Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwa chini ya mtini nilikuona. Nathanaeli akamjibu, Rabi, wewe u Mwana wa Mungu, ndiwe Mfalme wa Israeli. Yesu akajibu, akamwambia, kwa sababu nilikuambia, Nilikuona chini ya mtini, waamini? Utaona mambo makubwa kuliko haya. Akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Mtaziona mbingu zimefunguka na malaika wa Mungu wakikwea na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.

Maoni


Ingia utoe maoni