Masomo ya Misa
Jumanne ya 26 ya Mwaka (Jumanne, Septemba 27, 2022)
Ayu 3:1-3, 11-17, 20-23
Ayubu alifunua kinywa chake, na kuilaani siku yake. Ayubu akajibu, na kusema; Na ipotelee mbali ile siku niliyozaliwa mimi, Na ule usiku uliosema, Mtoto mume ametungishwa mimba. Mbona si kufa mimi tokea mimbani? Mbona nisitoe roho hapo nilipotoka tumboni? Mbona hayo magoti kunipokea? Au hayo maziwa, hata nikanyonya? Maana hapo ningelala na kutulia; Ningelala usingizi; na kupata kupumzika; Pamoja na wafalme na washauri wa dunia, Hao waliojijengea maganjoni; Au pamoja na wakuu wenye dhahabu, Waliozijaza fedha nyumba zao; Au, kama kuzikwa mimba iliyoharibika, nisingekuwako; Kama wachanga wasiouona mwanga kabisa. Huko waovu huacha kusumbua; Huko nako hao waliochoka wapumzika Mbona yeye aliye mashakani kupewa mwanga, Na hao wenye uchungu rohoni kupewa uhai; Ambao wangojea mauti, lakini hawayapati; Na kuyachimbulia zaidi ya kutafuta hazina iliyostirika; Ambao wafurahi mno, Na kushangilia watakapoliona kaburi? Kwa nini mtu aliyezibiwa njia kupewa mwanga, Ambaye Mungu amemzingira kwa ukingo?
Zab 88:1-7
Ee Bwana, Mungu wa wokovu wangu Mchana na usiku nimelia mbele zako.
Maombi yangu yafike mbele zako, Uutegee ukelele wangu sikio lako.
(K) Maombi yangu yafike mbele zako, Ee Bwana.
Maana nafsi yangu imeshiba taabu, Na uhai wangu umekaribia kuzimu.
Nimehesabiwa pamoja nao washukao shimoni; Nimekuwa kama mtu asiye na msaada.
(K) Maombi yangu yafike mbele zako, Ee Bwana.
Miongoni mwao waliokufa nimetupwa, Kama waliouawa walalao makaburini.
Hao ambao Wewe huwakumbuki tena, Wametengwa mbali na mkono wako.
(K) Maombi yangu yafike mbele zako, Ee Bwana.
Mimi umenilaza katika shimo la chini, Katika mahali penye giza vilindini.
Ghadhabu yako imenilemea, Umenitesa kwa mawimbi yako yote.
(K) Maombi yangu yafike mbele zako, Ee Bwana.
Mk 10:45
Aleluya, aleluya
Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.
Aleluya
Lk 9:51-56
Ilikuwa , siku za kupaa kwake zilipokuwa karibu kutimia, yeye aliukaza uso wake kwenda Yerusalemu; akatuma wajumbe kutangulia mbele ya uso wake; wakaenda wakaingia katika kijiji cha Wasamaria, ili kumtengenezea mahali. Lakini wenyeji hawakumkaribisha kwa vile alivyouelekeza uso wake kwenda Yerusalemu. Wanafunzi wake Yakobo na Yohana walipoona hayo, walisema, Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize; [kama Eliya naye alivyofanya]? Akawageukia, akawakanya. [Akasema, Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo.] Kwa maana Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa. Wakaondoka wakaenda mpaka kijiji kingine.
Maoni
Ingia utoe maoni