Jumamosi. 20 Aprili. 2024

Masomo ya Misa

Jumamosi ya 25 ya Mwaka (Jumamosi, Septemba 24, 2022)  

Somo la 1

Mh 11:9-12:8

Wewe kijana, uufurahie ujana wako, na moyo wako ukuchangamshe siku za ujana wako, ukaziendee njia za moyo wako, na katika maono ya macho yako, lakini ujue wewe ya kwamba kwa ajili ya hayo yote Mungu atakuleta hukumuni. Kwa hiyo ondoa majonzi moyoni mwako, nawe uuondoe ubaya mwilini mwako; kwa maana ujana ni ubatili, na utu uzima pia.Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo. Kabla jua, na nuru, na mwezi, Na nyota, havijatiwa giza; Kabla ya kurudi mawingu baada ya mvua; Siku ile walinzi wa nyumba watakapotetema; Hapo wenye nguvu watakapojiinamisha; Na wasagao kukoma kwa kuwa ni haba; Na hao wachunguliao madirishani kutiwa giza; Na milango kufungwa katika njia kuu; Sauti ya kinu itakapokuwa ni ndogo; Na mtu kusituka kwa sauti ya ndege; Nao binti za kuimba watapunguzwa; Naam, wataogopa kilichoinuka Na vitisho vitakuwapo njiani; Na mlozi utachanua maua; Na panzi atakuwa ni mzigo mzito; Na pilipili hoho itapasuka; Maana mtu aiendea nyumba yake ya milele, Nao waombolezao wazunguka njiani. Kabla haijakatika kamba ya fedha; Au kuvunjwa bakuli la dhahabu; Au mtungi kuvunjika kisimani; Au gurudumu kuvunjika birikani; Nayo mavumbi kuirudia nchi kama yalivyokuwa, Nayo roho kumrudia Mungu aliyeitoa. Mhubiri asema, Ubatili mtupu; mambo yote ni ubatili!

Wimbo wa Katikati

Zab 90:3-6, 12-14, 17

Wamrudisha mtu mavumbini, usemapo,
Rudini, enyi wanadamu.
Maana miaka elfu machoni pako
Ni kama siku ya jana ikiisha kupita,
Na kama kesha la usiku.
(K) Wewe Bwana, umekuwa makao yetu, kikazi baada ya kizazi.

Wawagharikisha, huwa kama usingizi,
Asubuhi huwa kama majani yameayo.
Asubuhi yachipuka na kumea,
Jioni yakatika na kukauka.
(K) Wewe Bwana, umekuwa makao yetu, kikazi baada ya kizazi.

Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu,
Tujipatie moyo wa hekima.
Ee Bwana urudi, hata lini?
Uwahurumie watumishi wako.
(K) Wewe Bwana, umekuwa makao yetu, kikazi baada ya kizazi.

Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako,
Nasi tutashangilia na kufurahi siku zetu zote.
Na uzuri wa Bwana, Mungu wetu, uwe juu yetu,
Na kazi ya mikono yetu utufanyie thabiti,
Naam, kazi ya mikono yetu uithibitishe.
(K) Wewe Bwana, umekuwa makao yetu, kikazi baada ya kizazi.

Shangilio

2Tim 1:10

Aleluya, aleluya
Mwokozi wetu Kristo Yesu; aliyebatili mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika, kwa ile Injili;
Aleluya

Injili

Lk 9:43-45

Makutano walipokuwa wakiyastaajabia mambo yote aliyoyafanya, Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Yashikeni maneno haya masikioni mwenu, kwa kuwa Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu. Lakini hawakulifahamu neno lile, likafichwa kwao wasilitambue; wakaogopa kumwuliza maana yake neno lile.

Maoni

LAULIANO MWALONGO

Endelea kubarikiwa

Ingia utoe maoni