Jumanne. 30 Mei. 2023

Masomo ya Misa

Ijumaa ya 25 ya Mwaka (Ijumaa, Septemba 23, 2022)  

Somo la 1

Mhu 3:1–11

Kwa kila jambo kuna majira yake, na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa; wakati wa kupanda, na wakati wa kung’oa yaliyopandwa; wakati wa kuua, na wakati wa kupoza; wakati wa kubomoa, na wakati wa kujenga; wakati wa kulia, na wakati wa kucheka; wakati wa kuomboleza, na wakati wa kucheza; wakati wa kutupa mawe, na wakati wa kukusanya mawe; wakati wa kukumbatia, na wakati wa kutokumbatia; wakati wa kutafuta, na wakati wa kupoteza; wakati wa kuweka, na wakati wa kutupa; wakati wa kurarua, na wakati wa kushona; wakati wa kunyamaza, na wakati wa kunena; wakati wa kupenda, na wakati wa kuchukia; wakati wa vita, na wakati wa amani. Je! Mtendaji anayo faida gani katika yale anayojishughulisha nayo? Nimeiona taabu ambayo Mungu amewapa wanadamu, ili kutaabika ndani yake. Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao; ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu mwanzo hata mwisho.

Wimbo wa Katikati

Zab 144:1–4

Ahimidiwe Bwana, mwamba wangu,
Mhisani wangu na boma langu,
Ngome yangu na mwokozi wangu,
Ngao yangu niliyemkimbilia.
(K) Ahimidiwe Bwana, mwamba wangu.

Ee Bwana, mtu ni kitu gani hata umjue?
Na binadamu hata umwangalie?
Binadamu amefanana na ubatili,
Siku zake ni kama kivuli kipitacho.
(K) Ahimidiwe Bwana, mwamba wangu.

Shangilio

Zab 119:135

Aleluya, aleluya,
Umwangazie mtumishi wako uso wako, na kunifundisha amri zako.
Aleluya.

Injili

Lk 9:18–22

Yesu alipokuwa akisali kwa faragha, wanafunzi wake walikuwapo pamoja naye, akawauliza, Je! Makutano hao wanasema ya kuwa mimi ni nani? Wakamjibu wakisema, Yohane Mbatizaji; lakini wengine, Eliya; na wengine kwamba mmojawapo wa manabii wa kale amefufuka. Akawaambia, Nanyi mwasema ya kwamba mimi ni nani? Petro akamjibu akasema, Ndiwe Kristo wa Mungu. Akawaonya, akawakataza wasimwambie mtu neno hilo. Akisema, Imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi, na kukataliwa na wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka.

Maoni


Ingia utoe maoni