Ijumaa. 19 Aprili. 2024

Masomo ya Misa

Alhamisi ya 25 ya Mwaka (Alhamisi, Septemba 22, 2022)  

Somo la 1

Mhu 1:1–11

Mhubiri asema, ubatili mtupu, ubatili mtupu, mambo yote ni ubatili. Mtu ana faida gani ya kazi yake yote aifanyayo chini ya jua? Kizazi huenda, kizazi huja; naye dunia hudumu daima. Jua lachomoza, na jua lashuka, na kufanya haraka kwenda mahali pa mawio yake. Upepo huvuma kusi, hugeuka kuwa kaskazi; hugeuka daima katika mwendo wake, na upepo huyarudia mazunguko yake. Mito yote huingia baharini, walakini bahari haijai; huko iendako mito, ndiko irudiko tena. Mambo yote yamejaa uchovu usioneneka, jicho halishibi kuona, wala sikio halikinai kusikia. Yaliyokuwako ndiyo yatakayokuwako; na yaliyotendeka ndiyo yatakayotendeka; wala jambo jipya hakuna chini ya jua. Je! Kuna jambo lolote ambalo watu husema juu yake, tazama, ni jambo jipya? Limekwisha kuwako, tangu zamani za kale zilizokuwa kabla yetu sisi. Hakuna kumbukumbu lolote la vizazi vilivyotangulia; wala hakutakuwa na kumbukumbu lolote la vizazi vitakavyokuja, miongoni mwao wale watakaofuata baadaye.

Wimbo wa Katikati

Zab 90:3–6, 12–14, 17

Wamrudisha mtu mavumbini,
Usemapo, Rudini, enyi wanadamu.
Maana miaka elfu machoni pako
Ni kama siku ya jana ikiisha kupita,
Na kama kesha la usiku.
(K) Wewe, Bwana, umekuwa makao yetu, kizazi baada ya kizazi.

Wawagharikisha, huwa kama usingizi,
Asubuhi huwa kama majani yameayo.
Asubuhi yachipuka na kumea,
Jioni yakatika na kukauka.
(K) Wewe, Bwana, umekuwa makao yetu, kizazi baada ya kizazi.

Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu,
Tujipatie moyo wa hekima.
Ee Bwana, urudi, hata lini?
Uwahurumie watumishi wako.
(K) Wewe, Bwana, umekuwa makao yetu, kizazi baada ya kizazi.

Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako,
Nasi tutashangilia na kufurahi siku zetu zote.
Na uzuri wa Bwana, Mungu wetu, uwe juu yetu,
Na kazi ya mikono yetu utufanyie thabiti.
(K) Wewe, Bwana, umekuwa makao yetu, kizazi baada ya kizazi.

Shangilio

Zab 27:11

Aleluya, aleluya,
Ee Bwana, unifundihse njia yako, na kuniongoza katika njia iliyonyoka.
Aleluya.

Injili

Lk 9:7–9

Herode mfalme alisikia habari za yote yaliyotendeka, akafadhaika kwa sababu watu wengine walisema ya kwamba Yohane amefufuka katika wafu, na wengine ya kwamba Eliya ametokea, na wengine ya kwamba mmojawapo wa manabii wa kale amefufuka. Lakini Herode akasema, Yohane nilimkata kichwa; basi ni nani huyu ambaye ninasikia mambo haya juu yake? Akataka kumwona.

Maoni


Ingia utoe maoni