Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 24 ya Mwaka (Jumapili, Septemba 11, 2022)  

Somo la 1

Kut 32:7-11, 13-14

Bwana alimwambia Musa, Haya! Shuka; kwa maana watu wako uliowatoa katika nchi ya Misri wamejiharibu nafsi zao, wamepotoka upesi kuiacha ile njia niliyowaamuru, wamejifanyizia ndama ya kuyeyusha wakaiabudu na kuitolea dhabihu, wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri. Tena Bwana akamwambia Musa, Mimi nimewaona watu hawa, na tazama, ni watu wenye shingo ngumu basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize, nami nitakufanya wewe uwe taifa kuu. 11 Musa akamsihi sana Bwana, Mungu wake, na kusema, Bwana, kwa nini hasira zako kuwaka juu ya watu wako uliowaleta kutoka nchi ya Misri kwa uweza mkuu, na kwa mkono wenye nguvu? Mkumbuke Ibrahimu, na Isaka, na Israeli, watumishi wako, ambao uliwaapia kwa nafsi yako, na kuwaambia, Nitazidisha kizazi chenu mfano wa nyota za mbinguni; tena nchi hii yote niliyoinena nitakipa kizazi chenu nao watairithi milele. Na Bwana akaughairi ule uovu aliosema ya kwamba atawatenda watu wake.

Wimbo wa Katikati

Zab 51: 1-2, 10-11, 15, 17

Ee Mungu, unirehemu,
Sawasawa na fadhili zako.
Kiasi cha wingi wa rehema zako,
Uyafute makosa yangu.
Unioshe kabisa na uovu wangu,
Unitakase dhambi zangu.
(K) Nitaondoka nitakwenda kwa baba yangu.

Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu
Usinitenge na uso wako,
Wala roho yako mtakatifu usiniondolee.
(K) Nitaondoka nitakwenda kwa baba yangu.

Ee Bwana, uifumbue midomo yangu,
Na kinywa changu kitazinena sifa zako.
Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika;
Moyo uliovunjika na kupondeka,
Ee Mungu, hutaudharau.
(K) Nitaondoka nitakwenda kwa baba yangu.

Somo la 2

1 Tim 1:12-17

Nami namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu kwa sababu aliniona kuwa mwaminifu, akaniweka katika utumishi wake; ingawa hapo kwanza nalikuwa mtukanaji, mwenye kuudhi watu, mwenye jeuri, lakini nalipata rehema kwa kuwa nalitenda hivyo kwa ujinga, na kwa kutokuwa na imani. Na neema ya Bwana wetu ilizidi sana, pamoja na imani na pendo lililo katika Kristo Yesu. Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa, ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi; ambao wa kwanza wao ni mimi. Lakini kwa ajili hii nalipata rehema, ili katika mimi wa kwanza, Yesu Kristo audhihirishe uvumilivu wake wote; niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini baadaye, wapate uzima wa milele. Sasa kwa Mfalme wa milele, asiyeweza kuona uharibifu, asiyeonekana, Mungu peke yake, na iwe heshima na utukufu milele na milele. Amina.

Shangilio

Yn 14:6

Aleluya, aleluya
Mimi ndimi Njia, na Ukweli na Uzima, asema Bwana; Mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
Aleluya

Injili

Lk 15:1-32

Watoza ushuru wote na wenye dhambi walikuwa wakimkaribia wamsikilize. Mafarisayo na waandishi wakanung'unika, wakisema, Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao. Akawaambia mfano huu, akisema, Ni nani kwenu, mwenye kondoo mia, akipotewa na mmojawapo, asiyewaacha wale tisini na kenda nyikani, aende akamtafute yule aliyepotea hata amwone? Naye akiisha kumwona, humweka mabegani pake akifurahi. Na afikapo nyumbani kwake, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimekwisha kumpata kondoo wangu aliyepotea. Nawaambia, Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu. Au kuna mwanamke gani mwenye shilingi kumi, akipotewa na moja, asiyewasha taa na kufagia nyumba, na kutafuta kwa bidii hata aione? Na akiisha kuiona, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimeipata tena shilingi ile iliyonipotea. Nawaambia, Vivyo hivyo kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye. Akasema, Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; yule mdogo akamwambia babaye, Baba, nipe sehemu ya mali inayoniangukia. Akawagawia vitu vyake. Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati. Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa kuu iliingia nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji. Akaenda akashikamana na mwenyeji mmoja wa nchi ile; naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe. Akawa akitamani kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, wala hapana mtu aliyempa kitu. Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa. Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako. Akaondoka, akaenda kwa babaye. Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana. Yule mwana akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena. Lakini baba aliwaambia watumwa wake, Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni; mleteni ndama yule aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi; kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana. Wakaanza kushangilia. Basi, yule mwanawe mkubwa alikuwako shamba na alipokuwa akija na kuikaribia nyumba, alisikia sauti ya nyimbo na machezo. Akaita mtumishi mmoja, akamwuliza, Mambo haya, maana yake nini? Akamwambia, Ndugu yako amekuja, na baba yako amemchinja ndama aliyenona, kwa sababu amempata tena, yu mzima. Akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi babaye alitoka nje, akamsihi. Akamjibu baba yake, akasema, Tazama, mimi nimekutumikia miaka mingapi hii, wala sijakosa amri yako wakati wo wote, lakini hujanipa mimi mwana-mbuzi, nifanye furaha na rafiki zangu; lakini, alipokuja huyu mwana wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona. Akamwambia, Mwanangu, wewe u pamoja nami sikuzote, na vyote nilivyo navyo ni vyako. Tena, kufanya furaha na shangwe ilipasa, kwa kuwa huyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.

Maoni

Cosmas Dohho

MUNGU awabariki Sana nimefarijiwa na masomo

Ingia utoe maoni