Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumatano ya 23 ya Mwaka (Jumatano, Septemba 07, 2022)  

Somo la 1

1Kor 7:25–31

Kwa habari za wanawali sina amri ya Bwana, lakini natoa shauri langu, mimi niliyejaliwa kwa rehema za Bwana kuwa mwaminifu. Basi, naona hili kuwa jema, kwa ajili ya shida iliyopo, kwamba ni vema mtu akae kama alivyo. Je! Umefungwa kwa mke? Usitake kufunguliwa. Umefunguliwa? Usitafute mke. Lakini, kama ukioa, huna hatia; wala mwanamwamli akiolewa, hana hatia; lakini watu kama hao watakuwa na dhiki katika mwili; name nataka kuwazuilia hayo. Lakini, ndugu, nasema hivi, muda ubakio si mwingi; basi tokea sasa wale walio na wake na wawe kama hawana; na wale waliao kama hawalii; na wale wafurahio kama hawafurahi; na wale wanunuao, kama hawana kitu. Na wale wautumiao ulimwengu huu, kama hawautumii sana; kwa maana mambo ya ulimwengu huu yanapita.

Wimbo wa Katikati

Zab 45:10–11, 13–16

Sikia, binti, utazame, utege sikio lako,
Uwasahau watu wako na nyumba ya baba yako.
Naye mfalme atautamani uzuri wako,
Maana ndiye bwana wako, nawe umsujudie.
(K) Sikia, binti, utazame, utege sikio lako.

Binti mfalme yumo ndani ana fahari tupu,
Mavazi yake ni nyuzi za dhahabu.
Atapelekwa kwa mfalme
Wanawali wenzake wanaomfuata.
(K) Sikia, binti, utazame, utege sikio lako.

Watapelekwa kwa furaha na shangwe,
Na kuingia katika nyumba ya mfalme.
Badala ya baba zako watakuwapo watoto wako,
Utawafanya kuwa wakuu katika nchi zote.
(K) Sikia, binti, utazame, utege sikio lako.

Shangilio

Zab 119:105

Aleluya, aleluya,
Neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu.
Aleluya.

Injili

Lk 6:20–26

Yesu aliinua macho yake akawatazama wanafunzi wake, akasema, Heri ninny imlio maskini, kwa sababu ufalme wa Mungu ni wenu. Heri ninyi mlio na njaa sasa, kwa sababu mtashiba. Heri ninyi mliao sasa, kwa sababu mtacheka. Heri ninyi watu watakapowachukia na kuwatenga, na kuwashutumu, na kulitupa nje jina lenu kama neno ovu, kwa ajili ya Mwana wa Adamu. Furahiwani siku ile na kuruka-ruka, kwa kuwa, tazama, thawabu yenu ni kubwa mbinguni; maana, baba zao waliwatenda manabii vivyo hivyo. Lakini, ole wenu ninyi mlio na mali, kwa kuwa faraja yenu mmekwisha kuipata. Ole wenu ninyi ambao mmeshiba sasa, kwa kuwa mtaona njaa. Ole wenu ninyi mnaocheka sasa, kwa kuwa mtaomboleza na kulia. Ole wenu ninyi watu wote watakapowasifu, kwa kuwa baba zao waliwatenda manabii wa uongo mambo kama hayo.

Maoni


Ingia utoe maoni