Masomo ya Misa
Jumanne ya 23 ya Mwaka (Jumanne, Septemba 06, 2022)
1Kor 6:1–11
Je! Mtu wa kwenu akiwa ana daawa juu ya mwenzake athubutu kushitaki mbele ya wasio haki, wala si mbele ya watakatifu? Au hamjui ya kwamba watakatifu watauhukumu ulimengu? Na ikiwa ulimwengu utahukumiwa na ninyi, je! Hamstahili kukata hukumu zilizo ndogo? Hamjui ya kuwa tutawahukumu malaika, basi si Zaidi sana na mambo ya maisha haya? Basi, mkiwa na mahali panapohukumiwa mambo ya maisha haya, mwawaweka kuwa waamuzi hao waliohesabiwa kuwa si kitu katika kanisa? Nasema hayo nipate kuwatahayarisha. Je! Ndivyo, kwamba kwenu hakuna hata mtu mmoja mwenye hekima, awezaye kukata maneno ya ndugu zake? Bali mwashitakiana, ndugu kwa ndugu, tena mbele yao wasioamini. Basi imekuwa upungufu kwenu kabisa kwamba mnashitakiana ninyi kwa ninyi wenyewe mwadhulumu watu na kunyang’anya mali zao; naam, hata za ndugu zenu. Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang’anyi. Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana Yesu Kristo, na katika Roho wa Mungu wetu.
Zab 149:1–6, 9
Aleluya.
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Sifa zake katika kusanyiko la watauwa.
Israeli na amfurahie Yeye aliyemfanya,
Wana wa SAyuni na wamshangilie mfalme wao.
(K) Bwana awaridhia watu wake.
Na walisifu jina lake kwa kucheza,
Kwa matari na kinubi wamwimbie.
Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake,
Huwapamba wenye upole kwa wokovu.
(K) Bwana awaridhia watu wake.
Watauwa na waushangilie utukufu,
Waimbe kwa sauti kuu vitandani mwao.
Sifa kuu za Mungu na ziwe vinywani mwao,
Hiyo ndiyo heshima ya watauwa wake wote.
Aleluya.
(K) Bwana awaridhia watu wake.
Zab 111:7, 8
Aleluya, aleluya,
Maagizo yako yote, Ee Bwana, ni amini, yamethibitika milele na milele.
Aleluya.
Lk 6:12–19
Yesu aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu. Hata kulipokuwa mchana aliwaita wanafunzi wake; akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita Mitume; Simoni, aliyemwita jina la pili Petro, na Andrea nduguye, na Yakobo na Yohane, na Filipo na Bartolomayo, na Mathayo na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Simoni aitwaye Zelote, na Yuda wa Yakobo, na Yuda Iskariote, ndiye aliyekuwa msaliti. Akashuka pamoja nao, akasimama mahali tambarare, pamoja na wanafunzi wake wengi, na makutano makubwa ya watu waliotoka Uyahudi wote na Yerusalemu, na pwani ya Tiro na Sidoni; waliokuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao; na wale waliosumbuliwa na pepo wachafu; waliponywa. Na makutano yote walikuwa wakitaka kumgusa, kwa sababu uweza ulikuwa ukimtoka ukiwaponya wote.
Maoni
Ingia utoe maoni