Masomo ya Misa
Jumamosi ya 20 ya Mwaka (Jumamosi, Agosti 20, 2022)
Eze 43:1–7
Bwana alinileta mpaka langoni, yaani, lango lile lielekealo upande wa mashariki; na tazama, huo utukufu wa Mungu wa Israeli ulitokea kwa njia ya mashariki; na sauti yake ilikuwa kama mshindo wa maji mengi, nayo nchi iling’aa kwa utukufu wake. Na maono niliyoyaona yalikuwa kama maono niliyoyaona nilipokuja kuuharibu mji; nayo maono niliyoyaona yalikuwa kama maono niliyoyaona karibu na mto wa Kebari; nikaanguka kifudifudi. Na huo utukufu wa Bwana ukaingia ndani ya nyumba, kwa njia ya lango lile lielekealo upande wa mashariki. Kisha Roho ikaniinua, ikanichukua mpaka ua wa ndani; na tazama, utukufu wa Bwana uliijaza nyumba. Nikasikia sauti ya mmoja asaemaye nami, itokayo katika nyumba hiyo; na mtu akasimama karibu nami. Akaniambia, Mwanadamu, hapa ni mahali pa kiti changu cha enzi, na mahali pa nyayo za miguu yangu, nitakapokaa kati ya wana wa Israeli milele.
Zab 85:8–13
Na nisikie atakavyosema Mungu Bwana,
Maana atawaambia watu wake Amani,
Naam, na watauwa wake pia,
Bali wasiurudie upumbavu tena.
Hakika wokovu wake u karibu na wamchao,
Utukufu ukae katika nchi yetu.
(K) Utukufu wa Bwana ukae katika nchi yetu.
Fadhili na kweli zimekutana,
Haki na Amani zimebusiana.
Kweli imechipuka katika nchi,
Haki imechungulia kutoka mbinguni.
(K) Utukufu wa Bwana ukae katika nchi yetu.
Naam, Bwana atatoa kilicho chema,
Na nchi yentu itakwenda mbele zake.
Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia.
(K) Utukufu wa Bwana ukae katika nchi yetu.
Zab 119:105
Aleluya, aleluya,
Neno lako nit aa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu.
Aleluya.
Mt 23:1–12
Yesu aliwambia makutano na wanafunzi wake, akasema, Waandishi na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Musa; basi, yoyote watakayowaambia, myashike, na kuyatenda; lakini kwa mfano wa matendo yao, msitende; maana wao hunena lakini hawatendi. Wao hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani mwao; wasitake wenyewe kuigusa kwa kidole chao. Tena matendo yao yote huyatenda ili kutazamwa na watu; kwa kuwa hupanua hirizi zao, huongeza matamvua yao; hupenda viti vya mbele katika karamu, na kuketi mbele katika masinagogi, na kusalimiwa masokoni, na kuitwa na watu, Rabi. Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu. Wala msimwite mtu baba duniani; maana Baba yenu ni mmoja, aliye wa mbinguni. Wala msiitwe viongozi; maana kiongozi wenu ni mmoja, naye ndiye Kristo. Naye aliye mkubwa wenu atakuwa mtumishi wenu. Na yeyote atakayejikweza, atadhiliwa; na yeyote atakayejidhili, atakwezwa.
Maoni
Ingia utoe maoni