Masomo ya Misa
Dominika ya 20 ya Mwaka (Jumapili, Agosti 14, 2022)
Yer 38:4–6, 8–10
Ndipo wakuu walimwambia mfalme, Twakuomba, mtu huyu auawe, kwa kuwa aidhoofisha mikono ya watu wa vita, waliobaki katika mji huu, na mikono ya watu wote, kwa kuwaambia maneno kama hayo; maana mtu huyu hawatafutii watu hawa heri, bali shari. Naye mfalme Sedekia akasema, Tazama, yu mikononi mwenu; maana mfalme siye awezaye kufanya neno lolote kinyume chenu. Basi wakamtwaa Yeremia, wakamtupa katika shimo la Malkiya, mwana wa mfalme, lililo katika uwanda wa walinzi; wakamshusha kwa kamba. Na mle shimoni hamkuwa na maji, ila matope tu; naye Yeremia akazama katika matope hayo. Ebedmeleki akatoka nyumbani mwa mfalme, akamwambia mfalme, akisema, Ee Bwana wangu, mfalme, watu hawa wametenda mabaya katika mambo yote waliyomtenda Yeremia, nabii, ambaye wamemtupa shimoni; naye hakosi atakufa pale alipo, kwa sababu ya njaa; kwa kuwa hapana mkate kabisa katika mji. Ndipo mfalme akamwamuru Ebedmeleki, Mkushi, akisema, chukua pamoja nawe watu thelathini; toka hapa, ukamtoe Yeremia shimoni, kabla hajafa.
Zab 40:1–3, 17
Nalimngoja Bwana kwa saburi,
Akaniinamia akakisikia kilio changu.
(K) Ee Bwana, unisaidie hima
Akanipandisha toka shimo la uharibifu,
Toka udongo wa utelezi;
Akaisimamisha miguu yangu mwambani,
Akaziimarisha hatua zangu.
(K) Ee Bwana, unisaidie hima
Akatia wimbo mpya kinyani mwangu,
Ndiyo sifa zake Mungu wetu.
Wengi wataona na kuogopa,
Nao watamtumaini Bwana.
(K) Ee Bwana, unisaidie hima
Nami ni maskini namhitaji,
Bwana atanitunza.
Ndiwe msaada wangu na wokovu wangu,
Ee Mungu wangu, usikawie.
(K) Ee Bwana, unisaidie hima
Ebr 12:1–4
Sisi pia kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu, tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. Maana mtafakarini sana yeey aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu. Hamjafanya vita hata kumwagika damu, mkishindana na dhambi.
Lk 19:38
Aleluya, aleluya,
Ndiye mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana; Amani mbinguni, na utukufu huko juu.
Aleluya.
Lk 12:49–53
Siku ile Yesu aliwaambia makutano: Nimekuja kutupa moto duniani; na ukiwa umekwisha washwa, ni nini nitakalo zaidi? Lakini nina ubatizo unipasao kubatizwa, nami nina dhiki kama nini hata utimizwe? Je! Mwadhani ya kwamba nimekuja kuleta amani duniani? Nawaambia, La, sivyo, bali mafarakano. Kwa kuwa tokea sasa katika nyumba moja watakuwamo watu watano wamefarakana, watatu kwa wawili, wawili kwa watatu. Watafarakana baba na mwanawe, na mwana na babaye; mama na binti yake, na binti na mamaye; mkwe mtu na mkwewe; mkwe na mkwe mtu.
Maoni
Ingia utoe maoni