Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Sikukuu ya Kung'aa Bwana Wetu Yesu Kristu (Jumamosi, Agosti 06, 2022)  

Somo la 1

Dan 7:9-10, 13-14

Mimi nilitazama hata viti vya enzi vikawekwa, na mmoja aliye mzee wa siku ameketi; mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji, na nywele za kichwa chake kama sufu safi; kiti chake cha enzi kilikuwa miali ya moto, na gurudumu zake moto uwakao. Mto kama wa moto ukatoka ukapita mbele zake; maelfu elfu wakamtumikia, na elfu kumi mara elfu kumi wakasimama mbele zake; hukumu ikawekwa, na vitabu vikafunuliwa. Nikaona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo mzee wa siku, wakamleta karibu naye. Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa.

Wimbo wa Katikati

Zab 97:1-2, 5-6, 9

Bwana ametamalaki, nchi na ishangilie, Visiwa vingi na vifurahi.
Mawingu na giza vyamzunguka, Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chake.
(K)Bwana ni Mfalme, aliye juu sana kuliko nchi yote;

Milima iliyeyuka kama nta mbele za Bwana, Mbele za Bwana wa dunia yote.
Mbingu zimetangaza haki yake, Na watu wote wameuona utukufu wake.
(K)Bwana ni Mfalme, aliye juu sana kuliko nchi yote;

Maana Wewe, Bwana, ndiwe Uliye juu, Juu sana kuliko nchi yote;
Umetukuka sana juu ya miungu yote.
(K)Bwana ni Mfalme, aliye juu sana kuliko nchi yote;

Somo la 2

2 Pet 1:16-19

Maana hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu, tulipowajulisha ninyi nguvu zake Bwana wetu Yesu Kristo na kuja kwake; bali tulikuwa tumeuona wenyewe ukuu wake. Maana alipata kwa Mungu Baba heshima na utukufu, hapo alipoletewa sauti iliyotoka katika utukufu mkuu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Na sauti hiyo sisi tuliisikia ikitoka mbinguni tulipokuwa pamoja naye katika mlima ule mtakatifu. Nasi tuna lile neno la unabii lililo imara zaidi, ambalo, mkiliangalia, kama taa ing'aayo mahali penye giza, mwafanya vyema, mpaka kutakapopambazuka, na nyota ya asubuhi kuzuka mioyoni mwenu.

Shangilio

Mt 17:5c

Aleluya, aleluya
Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye.
Aleluya

Injili

Lk 9:28b-36

Yesu aliwatwaa Petro na Yohana na Yakobo, akapanda mlimani ili kuomba. Ikawa katika kusali kwake sura ya uso wake ikageuka, mavazi yake yakawa meupe, yakimeta-meta. Na tazama, watu wawili walikuwa wakizungumza naye, nao ni Musa na Eliya; walioonekana katika utukufu, wakanena habari za kufariki kwake atakakotimiza Yerusalemu. Petro na wale waliokuwa pamoja naye walikuwa wamelemewa na usingizi; lakini walipokwisha amka waliuona utukufu wake, na wale wawili waliosimama pamoja naye. Ikawa hao walipokuwa wakijitenga naye, Petro alimwambia Yesu, Bwana mkubwa, ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu; kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya; hali hajui asemalo. Alipokuwa akisema hayo, lilitokea wingu likawatia uvuli, wakaogopa walipoingia katika wingu hilo. Sauti ikatoka katika wingu, ikisema, Huyu ni Mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye. Na sauti hiyo ilipokwisha, Yesu alionekana yu peke yake. Nao wakanyamaza, wasitangaze kwa mtu siku zile lo lote katika hayo waliyoyaona.

Maoni


Ingia utoe maoni