Masomo ya Misa
Jumatatu ya 16 ya Mwaka (Jumatatu, Julai 18, 2022)
Mik 6:1–4, 6–8
Sikieni asemavyo Bwana; Simama, ujitetee mbele ya milima, vilima navyo na visikie sauti yako. Sikieni, enyi milima, mateto ya Bwana, na ninyi, enyi misingi ya dunia iliyo imara; kwa maana Bwana ana mateto na watu wake, naye atahujiana na Israeli. Enyi watu wangu, nimewatenda nini? Nami nimewachosha kwa habari gani? Shuhudieni juu yangu. Kwa maana nalikupandisha kutoka nchi ya Misri, na kukukomboa utoke katika nyumba ya utumwa, nami naliwapeleka Musa, na Haruni, na Miriamu, watangulie mbele yako. Nimkaribie Bwana na kitu gani, na kuinamana mbele za Mungu aliye juu? Je! Nimkaribie na sadaka za kuteketezwa, na ndama za umri wa mwaka mmoja? Je! Bwana atapendezwa na elfu za kondoo waume, au na elfu kumi za mito ya mafuta? Je! Nimtoe mzaliwa wangu wa kwanza kwa kosa langu, mzao wa mwili wangu kwa dhambi ya roho yangu? Ee mwanadamu, yeye amekuonyesha yaliyo mema; na Bwana anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako!
Zab 50:5–6, 8–9, 16–17, 21, 23
Nikusanyieni wacha Mungu wangu,
Waliofanya agano nami kwa dhabihu.
Na mbingu zitatangaza haki yake,
Kwa maana Mungu ndiye aliye hakimu.
(K)Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.
Sitakukemea kwa ajili ya dhabihu zako,
Na kafara zako ziko mbele zangu daima.
Sitatwaa ng’ombe katika nyumba yako,
Wala beberu katika mazizi yako.
(K)Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.
Mtu asiye haki, Mungu amwambia,
Una nini wewe kuitangaza sheria yangu.
Maana wewe umechukia maonyo,
Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako.
(K)Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.
Ndivyo ulivyofanya, nami nikanyamaza,
Ukadhani ya kuwa Mimi ni kama wewe.
Atoaye dhabihu za kushukuru ndiye anayenitukuza,
Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.
(K)Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.
Yn 17:17
Aleluya, aleluya,
Neno lako ndiyo kweli, ee Bwana, ututakase kwa ile kweli.
Aleluya.
Mt 12:38–42
Baadhi ya waandishi wa Mafarisayo walimjibu Yesu wakasema, Mwalimu, twataka kuona ishara kwako. Akajibu, akawaambia, Kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya nabii Yona. Kwani kama vile Yona alivyokuwa siku tatu mchana na usiku katika tumbo la nyangumi, hivyo ndivyo Mwana wa Adamu atakavyokuwa siku tatu mchana na usiku moyo wa nchi. Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, nao watawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona; na hapa yupo aliye mkuu kuliko Yona. Malkia wa kusini atasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu yeye alikuja kutoka pande za mwisho za dunia ili asikie hekima ya Sulemani, na hapa yupo aliye mkuu kuliko Sulemani.
Maoni
Ingia utoe maoni