Masomo ya Misa
Dominika ya 14 ya Mwaka (Jumapili, Julai 03, 2022)
Isa 66:10–14
Furahini pamoja na Yerusalemu, shangilieni kwa ajili yake, ninyi nyote mmpendao; furahini pamoja naye kwa furaha, ninyi nyote mliao kwa ajili yake; mpate kunyonya, na kushibishwa kwa maziwa ya faraja zake, mpate kukama, na kufurahiwa kwa wingi wa utukufu wake. Maana Bwana asema hivi, Tazama, nitamwelekezea Amani kama mto, na utukufu wa mataifa kama kijito kifurikacho, nanyi mtapata kunyonya; mtabebwa; na juu ya magoti mtabembelezwa. Mfano wa mtu ambaye mama yake amfariji, ndivyo nitakavyowafariji ninyi; nanyi mtafarijiwa katika Yerusalemu. Nanyi mtaona, na mioyo yenu itafurahi, na mifupa yenu itasitawi kama majani mabichi; na mkono wa Bwana utajulikana, uwaelekeao watumishi wake.
Zab 66:1–7, 16, 20
Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote,
Imbeni utukufu wa jina lake.
Tukuzeni sifa zake,
Mwambieni Mungu, matendo yako yanatisha kama nini!
(K) Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote.
Nchi yote itakusujudia na kukuimbia,
Naam, italiimbia jina lako.
Njoni yatazameni matendo ya Mungu,
Hutisha kwa mambo awatendayo wanadamu.
(K) Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote.
Aligeuza bahari ikawa nchi kavu;
Katika mto walivuka kwa miguu;
Huko ndiko tulikomfurahia,
Atawala kwa uweza wake milele.
(K) Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote.
Njoni, sikieni, ninyi nyote mnaomcha Mungu,
Name nitayatangaza aliyonitendea roho yangu.
Na ahimidiwe Mungu aliyeyakataa maombi yangu,
Wala kuniondolea fadhili zake.
(K) Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote.
Gal 6:14–18
Mimi, hasha, nisione fahari juu ya kito chochote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu. Kwa sababu kutahiriwa si kitu, wala kutokutahiriwa, bali kiumbe kipya. Na wote watakaoenenda kwa kanuni hiyo, Amani na iwe kwao rehema, naam, kwa Israeli wa Mungu. Tangu sasa mtu asinitaabishe; kwa maana ninachukua mwilini mwangu chapa zake Yesu. Ndugu zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja na roho zenu. Amina.
Yn 1:12, 14
Aleluya, aleluya,
Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu.
Aleluya.
Lk 10:1–12, 17–20
Baada ya hayo Bwana aliweka na wengine, sabini, akawatuma wawili wawili wamtangulie kwenye kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda mwenyewe. Akawaambia, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno apelike watenda kazi katika mavuno yake. Enendeni, angalieni, nawatuma kama wanakondoo kati ya mbwa-mwitu. Msichukue mfuko, wala mkoba, wala viatu; wala msimwamkie mtu njiani. Na nyumba yoyote mtakayoingia, semeni kwanza, Amani iwemo nyumbani humu; na akiwamo mwana wa Amani, Amani yenu itamkalia; la, hayumo, Amani yenu itarudi kwenu. Basi, kaeni katika nyumba iyo hiyo, mkila na kunywa vya kwao; maana, mtenda kazi amestahili kupewa ujira wake. Msihamehame kutoka nyumba hii kwenda nyumba hii. Na mji wowote mtakaouingia, wakiwakaribisha, vileni vyakula viwekwavyo mbele yenu; wapozeni wagonjwa waliomo, waambieni, Ufalme wa Mungu umewakaribia. Na mji wowote mtakaouingia, nao hawawakaribishi, tokeni humo, nanyi mkipita katika njia zake semeni, Hata mavumbi ya mji wenu yaliyogandamana na miguu yenu tunayakung’uta juu yenu. Lakini jueni hili, ya kuwa Ufalme wa Mungu umekaribia. Nawaambia ya kwamba siku ile itakuwa rahisi zaidi Sodoma kuistahimili adhabu yake kuliko mji huo. Ndipo wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako. Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme. Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru. Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahaini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.
Maoni
Ingia utoe maoni