Masomo ya Misa
Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba Mtakatifu (Jumatano, Septemba 14, 2016)
Hes. 21:4 – 9
Siku zile jangwani, watu walimnung’unikia Mungu, na Musa, mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu. Bwana akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa. Watu wakamwendea Musa, wakasema, tumefanya dambi kwa sababu tumemnung’unukia Mungu, na wewe, utuombee kwa Bwana, atuondolee nyoka hawa. Basi, Musa akawaombea watu. Bwana akawaambia Musa, Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo, ataishi. Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi.
Zab. 78:1 – 2, 34 – 38
Enyi watu wangu, sikilizeni sheria yangu,
Tegeni masikio kwa maneno ya kinywa changu.
Na nifunue kinywa changu kwa mithali,
Niyatamke mafumbo ya kale.
(K) Msiyasahau matendo ya Mungu.
Alipowaua ndipo walipokuwa wakimtafuta;
Wakarudi wakamtaka Mungu kwa bidii.
Wakakumbuka kuwa Mungu ni mwamba wao,
Na Mungu Aliye juu ni mkombozi wako.
(K) Msiyasahau matendo ya Mungu.
Lakini walimdanganya kwa vinywa vyao,
Wakamwambia uongo kwa ndimi zao.
Kwa maana mioyo yao haikuwa thabiti kwake,
Wala hawakuwa waaminifu katika agano lake.
(K) Msiyasahau matendo ya Mungu.
Lakini Yeye, kwa kuwa anayo rehema,
Husamehe uovu wala haangamizi.
Mara nyingi huipishia mbali ghadhabu yake,
Wala haiwashi hasira yake yote.
(K) Msiyasahau matendo ya Mungu.
Fil. 2:6 – 11
Yesu Kristo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama wanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mung alimwadhimisha mno, akamkirimia jina lile lipitalo kila jina, ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.
.
Aleluya, aleluya,
Ee Kristu tunakuabudu na kukutukuza,
kwa kuwa umeikomboa dunia kwa msalaba wako.
Aleluya.
Yn. 3:13 – 17
Yesu alimwambia Nikodemo: Hakuna mtu aliyepaa mbinguni, ila yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, Mwana wa Adamu. Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye. Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.
Maoni
Ingia utoe maoni