Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumanne ya 11 ya Mwaka (Jumanne, Juni 14, 2022)  

Somo la 1

1Fal 21:17-29

Neno la Bwana likamjia Eliya Mtishbi, kusema, Ondoka, ushuke, ukutane na Ahabu mfalme wa Israeli, akaaye katika Samaria; yuko katika shamba la mizabibu la Nabothi, ndiko alikoshukuia ili alitamalaki. Ukamwambie, ukisema, Bwana asema hivi, Je! Umeua, ukatamalaki? Nawe utamwambia, kusema, Bwana asema hivi, mahali pale mbwa walipoiramba damu ya Nabothi, mbwa watairamba na damu yako, naam, damu yako. Ahabu akamwambia Eliya, Je! Umenipata, ewe adui yangu? Akamwambia, Nimekupata, kwa sababu umejiuza utende yaliyo mabaya machoni pa Bwana. Angalia, nitaleta mabaya juu yako; nami nitakuangamiza kabisa, nitamkatia Ahabu kila mume, aliyefungwa na aliyeachwa katika Israeli. Kisha nitaifanya nyumba yako iwe kama nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebari, na kama nyumba ya Baasha mwana wa Ahiya, kwa ajili ya chukizo ulilonichukiza, hata kunighadhibisha, ukawakosesha Israeli. Tena Bwana alinena habari za Yezebeli, akisema, mbwa watamla Yezebeli katika kiwanja cha Yezreeli. Mtu wa nyumba ya Ahabu afanye mjini, mbwa watamla, na yeye afaye mashamba ndege wa angani watamla. Lakini hapakuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza atende maovu machoni pa Bwana, ambaye Yezebeli mkewe alimchochea. Akachukiza mno, kwa kuzifuata sanamu sawasawa na yote waliyoyafanya Waamori, Bwana aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli. Ikawa, Ahabu alipoyasikia maneno hayo, akayararua mavazi yake, akavaa magunia mwilini mwake, akafunga, akajilaza juu ya magunia, akaenda kwa upole. Neno la Bwana likaja kwa Eliya Mtishbi, kusema, Huoni jinsi Ahabu alivyojidhili mbele yangu? Basi kwa sababu amejidhili mbele yangu, sitayaleta yale mabaya katika siku zake; ila katika siku za mwanawe nitayaleta mabaya hayo juu ya nyumba yake.

Wimbo wa Katikati

Zab 51:1-4, 9, 15

Ee Mungu unirehemu, sawasawa na fadhili zako.
Kiasi cha wingi wa rehema zako,
Uyafute makosa yangu.
Unioshe kabisa na uovu wangu,
Unitakase dhambi zangu.
(K) Ee Mungu uturehemu uyafute makosa yetu.

Maana nimejua mimi makosa yangu,
Na dhambi yangu i mbele yangu daima.
Nimekutenda dhambi Wewe peke yako.
(K) Ee Mungu uturehemu uyafute makosa yetu.

Usitiri uso wako usitazame dhambi zangu,
Uzifute hatia zangu zote.
Ee Bwana, uifumbue midomo yangu,
Na kinywa hcangu kitazinena sifa zako.
(K) Ee Mungu uturehemu uyafute makosa yetu.

Shangilio

Yak 1:21

Aleluya, aleluya.
Pokeeni kwa upole neno la Mungu lililopandwa ndani, liwezalo kuiokoa roho zenu.
Aleluya.

Injili

Mt 5:43–48

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, pendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi; ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi, mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru; je! Nao hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo? Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.

Maoni


Ingia utoe maoni