Masomo ya Misa
Sikukuu ya Mt. Marko, Mwinjili (Jumatatu, Aprili 25, 2022)
1Pet 5:5-14
Ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema. Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu. Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze. Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kuwa mateso yale yale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani. Na Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele katika Kristo, mkiisha kuteswa kwa muda kidogo, yeye mwenyewe atawatengeneza, na kuwathibitisha, na kuwatia nguvu. Uweza una yeye hata milele na milele. Amina. Kwa mkono wa Silwano, ndugu mwaminifu kama nionavyo, nimewaandikia kwa maneno machache, kuonya na kushuhudia ya kuwa hii ndiyo neema ya kweli ya Mungu. Simameni imara katika hiyo. Mwenzenu mteule hapa Babeli awasalimu, na Marko mwanangu. Salimianeni kwa busu la upendo. Amani na iwe kwenu nyote, mlio katika Kristo. Amina.
Zab 89:1-2, 5-6, 15-16
Fadhili za Bwana nitaziimba milele;
Kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako.
Maana nimesema, Fadhili zitajengwa milele;
Katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako.
(K) Fadhili zako nitaziimba milele, Ee Bwana.
Ee Bwana, mbingu zitayasifu maajabu yako,
Uaminifu wako katika kusanyiko la watakatifu.
Maana ni nani katika mbingu awezaye kulinganishwa na Bwana?
Ni nani afananaye na Bwana miongoni mwa malaika?
(K) Fadhili zako nitaziimba milele, Ee Bwana.
Heri watu wale waijuao sauti ya shangwe,
Ee Bwana, huenenda katika nuru ya uso wako.
Kwa jina lako hufurahi mchana kutwa,
Na kwa haki yako hutukuzwa.
(K) Fadhili zako nitaziimba milele, Ee Bwana.
1Kor 1:23-24
Aleluya, aleluya,
Sisi tunamhubiri Kristu, aliyesulibiwa, ni nguvu na hekima ya Mungu.
Aleluya.
Mk 16:15-20
Yesu aliwaambia wale kumi na mmoja, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya. Basi Bwana Yesu, baada ya kusema nao, akachukuliwa juu mbinguni, akaketi mkono wa kuume wa Mungu. Nao wale wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo.
Maoni
Ingia utoe maoni