Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 1 ya Kwaresima (Jumapili, Machi 06, 2022)  

Somo la 1

Kumb. 26:4-10

Musa aliwaambia Waisraeli wote: Naye kuhani atakipokea kikapu mkononi mwako, akiweke chini mbele ya madhabahu ya Bwana, Mungu wako. Nawe ujibu, ukaseme mbele za Bwana, Mungu wako. Baba yangu alikuwa Mwarami karibu na kupotea, akashuka Misri akakaa huko ugenini, nao ni wachache hesabu yao; akawa taifa kubwa huko, yenye nguvu na watu wengi. Wamisri wakatuonea, wakatutesa, wakatutumikisha utumwa mzito. Tukamlilia Bwana, Mungu wa baba zetu; Bwana akasikia sauti yetu, akaona na taabu yetu, na kazi yetu, na kuonewa kwetu. Bwana akatutoa kutoka Misri kwa mkono wa nguvu, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa utisho mwingi, na kwa ishara, na kwa maajabu; naye ametuingiza mahali hapa, na kutupa nchi hii, nchi ijaayo maziwa na asali. Na sasa, tazama, nimeleta malimbuko ya mazao ya ardhi uliyonipa, Ee Bwana. Kisha ukiweke chini mbele za Bwana, Mungu wako, ukasujudu mbele za Bwana, Mungu wako.

Wimbo wa Katikati

Zab. 91:12, 10-15

Aketiye mahali pa siri pake Aliye juu,
Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi.
Nitasema, Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu.
(K) Ee Bwana, uwe pamoja nami katika taabu zangu.

Mabaya hayatakupata wewe,
Wala tauni haitaikaribia hema yako.
Kwa kuwa atakuagizia malaika zake
Wakulinde katika njia zako zote.
(K) Ee Bwana, uwe pamoja nami katika taabu zangu.

Mikononi mwao watakuchukua,
Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.
Utawakanyaga simba na nyoka,
Mwana-simba na joka utawaseta kwa miguu.
(K) Ee Bwana, uwe pamoja nami katika taabu zangu.

Kwa kuwa amekaza kunipenda
Nitamwokoa; na kumweka palipo juu,
Kwa kuwa amenijua jina langu.
Ataniita nami nitamwitikia;
Nitakuwa pamoja naye taabuni,
Nitamwokoa na kumtukuza.
(K) Ee Bwana, uwe pamoja nami katika taabu zangu.

Somo la 2

Rum. 10:10-13

Lakini yanenaye? Lile neno li karibu nawe, katika kinywa chako, na katika moyo wako; yaani, ni lile neno la Imani tulihubirilo. Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao; kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka.

Shangilio

Mt. 4:4

Mtu hataishi kwa mkate tu, Ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.

Injili

Lk. 4:1-13

Na Yesu, hali amejaa Roho Mtakatifu, alirudi kutoka Yordani, akaongozwa na Roho muda wa siku arobaini nyikani, akijaribiwa na Ibilisi. Na siku hizo alikuwa hali kitu; hata zilipotimia, aliona njaa. Ibilisi akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, liambie jiwe hili liwe mkate. Yesu akamjibu, imeandikwa ya kwamba mtu hataishi kwa mkate tu. Akampandisha juu, akamwonyesha milki zote za ulimwengu kwa dakika moja. Ibilisi akamwambia, Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa yeyote kama nipendavyo. Basi, wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako. Yesu akajibu akamwambia, Imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, mwambudu yeye peke yake. Akamwongoza mpaka Yerusalemu, akamweka juu ya kinara cha hekalu, akamwambia, Ukiwa ndiwe mwana wa Mungu, jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake wakulinde; ya kwamba, Mikononi mwao watakuchukua, Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. Yesu akajibu akamwambia, Imenenwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako. Basi alipomaliza kila jaribu, Ibilisi akamwacha aende zake kwa muda.

Maoni


Ingia utoe maoni