Masomo ya Misa
Alhamisi ya 6 ya Mwaka (Alhamisi, Februari 17, 2022)
Yak 2:1-9
Ndugu zangu, imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe nayo kwa kupendelea watu. Maana akiingia katika sinagogi lenu mtu mwenye pete ya dhahabu na mavazi mazuri; kisha akiingia na maskini, mwenye mavazi mabovu; nanyi mkimstahi yule aliyevaa mavazi mazuri, na kumwambia, Keti wewe hapa mahali pazuri; na kumwambia yule maskini, Simama wewe pale, au keti miguuni pangu, je! Hamkufanya hitilafu mioyoni mwenu, mkawa waamuzi wenye mawazo mabovu? Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni, Je! Mungu hakuwachagua maskini wa dunia wawe matajiri wa imani na warithi wa ufalme aliowaahidia wampendao? Bali ninyi mmemvunjia heshima maskini. Je! Matajiri hawawaonei ninyi na kuwavuta mbele ya viti vya hukumu? Hawalitukani jina lile zuri mliloitwa? Lakini mkiitimiza ile sheria ya kifalme kama ilivyoandikwa, Mpende jirani yako kama nafsi yako, mwatenda vema. Bali mkiwapendelea watu, mwafanya dhambi na kuhukumiwa na sheria kuwa wakosaji.
Zab 34:1-6
Nitamhimidi Bwana kila wakati,
Sifa zake zi kinywani mwangu daima.
Katika Bwana nafsi yangu itajisifu,
Wanyenyekevu wasikie wakafurahi.
(K) Maskini huyu aliita, Bwana akasikia
Mtukuzeni Bwana pamoja nami,
Na tuliadhimishe jina lake pamoja.
Nalimtafuta Bwana akanijibu,
Akaniponya na hofu zangu zote.
(K) Maskini huyu aliita, Bwana akasikia
Wakamwelekea macho wakatiwa nuru,
Wala nyuso zao hazitaona haya.
Maskini huyu aliita, Bwana akasikia,
Akamwokoa na taabu zake zote.
(K) Maskini huyu aliita, Bwana akasikia
Mk 8:27-33
Siku ile Yesu alitoka na wanafunzi wake, wakaenda kwenye vijiji vya Kaisaria-Filipi; na njiani akawauliza wanafunzi wake, akasema, Watu huninena mimi kuwa ni nani? Wakamjibu, Yohana Mbatizaji; wengine, Eliya; wengine, Mmojawapo wa manabii. Naye akawauliza, Na ninyi mnasema ya kuwa mimi ni nani? Petro akamjibu, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo. Akawaonya wasimwambie mtu habari zake. Akaanza kuwafundisha kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupatikana na mateso mengi, na kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na baada ya siku tatu kufufuka. Naye alikuwa akinena neno hilo waziwazi. Petro akamchukua, akaanza kumkemea. Akageuka, akawatazama wanafunzi wake, akamkemea Petro, akasema, Nenda nyuma yangu, Shetani; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.
Maoni
Ingia utoe maoni