Masomo ya Misa
Kutolewa Bwana Hekaluni (Jumatano, Februari 02, 2022)
Mal 3:1-4
Bwana Mungu asema hivi: Angalieni, namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia mbele yangu; naye Bwana mnayemtafuta atalijilia hekalu lake ghafula; naam, yule mjumbe wa agano mnayemfurahia, angalieni, anakuja, asema Bwana wa majeshi. Lakini ni nani atakayestahimili siku ya kuja kwake? Au ni nani atakayesimama atakapoonekana yeye? Kwa maana yeye ni mfano wa moto wa mtu asafishaye fedha, ni mfano wa sabuni ya mtu afuaye nguo; naye ataketi kama asafishaye fedha na kuitakasa, naye atawatakasa wana wa Lawi, atawasafisha kama dhahabu na fedha; nao watamtolea Bwana dhabihu katika haki. Wakati ule ndipo dhabihu za Yuda na Yerusalemu zitakapopendeza mbele za Bwana, kama katika siku za kale, na kama katika miaka ya zamani.
Zab 24:7-10
Inueni vichwa vyenu, enyi malango,
Inukeni, enyi malango ya milele,
Mfalme wa utukufu apate kuingia.
(K) Ni nani mfalme wa utukufu! Ni Bwana, mwenye nguvu, hodari
Ni nani Mfalme wa utukufu?
Bwana mwenye nguvu, hodari,
Bwana hodari wa vita.
(K) Ni nani mfalme wa utukufu! Ni Bwana, mwenye nguvu, hodari
Inueni vichwa vyenu, enyi malango,
Naam, viinueni, enyi malango ya milele,
Mfalme wa utukufu apate kuingia.
(K) Ni nani mfalme wa utukufu! Ni Bwana, mwenye nguvu, hodari
Ni nani huyu Mfalme wa utukufu?
Bwana wa majeshi,
Yeye ndiye Mfalme wa utukufu.
(K) Ni nani mfalme wa utukufu! Ni Bwana, mwenye nguvu, hodari
Ebr 2:14-18
Kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi, awaache huru wale ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa. Maana ni hakika, hatwai asili ya malaika, ila atwaa asili ya mzao wa Ibrahimu. Hivyo ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili afanye suluhu kwa dhambi za watu wake. Na kwa kuwa mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wao wanaojaribiwa.
Lk 2:32
Aleluya, aleluya!
Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli.
Aleluya!
Lk 2:22-40
Zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, (kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana), wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili. Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, Uliouweka tayari machoni pa watu wote; Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli. Na babaye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi. Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake. Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba. Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake. Basi, walipokwisha kuyatimiza yote kama yalivyoagizwa katika sheria ya Bwana, walirejea Galilaya mpaka mjini kwao, Nazareti. Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.
Maoni
Ingia utoe maoni