Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumatano ya 3 ya Majilio (Jumatano, Desemba 15, 2021)  

Somo la 1

Isa 45:6-8, 18-25

Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine. Mimi naiumba nuru, na kulihuluku giza; mimi nafanya suluhu, na kuhuluku ubaya; Mimi ni Bwana, niyatendaye hayo yote. Dondokeni, enyi mbingu, toka juu, Mawingu na yamwage haki; Nchi na ifunuke, ili kutoa wokovu, Nayo itoe haki ikamee pamoja; Mimi, Bwana, nimeiumba. Maana Bwana, aliyeziumba mbingu, asema hivi; Yeye ni Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu; Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine. Sikusema kwa siri, katika mahali pa nchi ya giza; sikuwaambia wazao wa Yakobo; Nitafuteni bure; Mimi, Bwana, nasema haki; nanena mambo ya adili. Jikusanyeni mje; na kukaribia pamoja, ninyi wa mataifa mliookoka; hawana maarifa wale wachukuao mti wa sanamu yao ya kuchonga; wamwombao mungu asiyeweza kuokoa. Hubirini, toeni habari; naam, na wafanye mashauri pamoja; ni nani aliyeonyesha haya tangu zamani za kale? Ni nani aliyeyahubiri hapo zamani? Si mimi, Bwana? Wala hapana Mungu zaidi ya mimi; Mungu mwenye haki, mwokozi; hapana mwingine zaidi ya mimi. Niangalieni mimi, mkaokolewe, enyi ncha zote za dunia; maana mimi ni Mungu; hapana mwingine. Kwa nafsi yangu nimeapa, neno hili limetoka kinywani mwangu katika haki, wala halitarudi, ya kwamba mbele zangu kila goti litapigwa, kila ulimi utaapa. Mmoja ataniambia, Kwa Bwana, peke yake, iko haki na nguvu; naam, watu watamwendea yeye, na wote waliomkasirikia watatahayarika. Katika Bwana wazao wote wa Israeli watapewa haki, na kutukuka.

Wimbo wa Katikati

Zab 85:8a, 9-13

Na nisikie atakavyosema Mungu Bwana,
Maana atawaambia watu wake amani,
Hakika wokovu wake u karibu na wamchao,
Utukufu ukae katika nchi yetu.
(K) Dondokeni, enyi mbingu, toka juu, Mawingu na yamwage haki

Fadhili na kweli zimekutana,
Haki na amani zimehusiana.
Kweli imechipuka katika nchi,
Haki imechungulia kutoka mbinguni.
(K) Dondokeni, enyi mbingu, toka juu, Mawingu na yamwage haki

Naam, Bwana atatoa kilicho chema,
Na nchi yetu itatoa mazao yake.
Haki itakwenda mbele zake,
Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia.
(K) Dondokeni, enyi mbingu, toka juu, Mawingu na yamwage haki

Shangilio

Isa 40:9–10

Aleluya, aleluya,
Paza sauti kwa nguvu, Wewe uhubiriye habari njema; Tazameni, Bwana Mungu atakuja kama shujaa.
Aleluya.

Injili

Lk 7:19-23

Siku ile Yohane alipowaita wawili katika wanafunzi wake, akawatuma kwa Yesu akiuliza, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine? Nao walipofika kwake, walisema, Yohane Mbatizaji ametutuma kwako, akisema, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine? Na saa ile ile aliwaponya wengi magonjwa yao, na misiba, na pepo wabaya; na vipofu wengi aliwakirimia kuona. Ndipo alipojibu, akawaambia, Nendeni mkamweleze Yohane hayo mliyoyaona na kuyasikia; vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakasika, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, maskini wanahubiriwa habari njema. Naye heri mtu ye yote asiyechukizwa nami.

Maoni


Ingia utoe maoni