Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 2 ya Majilio (Jumapili, Desemba 05, 2021)  

Somo la 1

Bar 5:1-9

Ee Yerusalemu, vua nguo za matanga na huzuni, Uvae uzuri wa utukufu utokao kwa Mungu milele. Jifungie nguo ya haki itokayo kwa Mungu, Jipige kilemba kichwani cha utukufu wake Aliye wa Milele. Maana Mungu ataidhihirisha nuru yako duniani mwote, Na jina lako litaitwa na Mungu daima, Amani ya haki, na Utukufu wa utauwa. Ondoka, Ee Yerusalemu, usimame juu; Tazama upande wa mashariki, uangalie: Toka macheo ya jua hata maawio yake wanao wanakusanyika kwa neno lake Yeye Aliye Mtakatifu, Wakifurahi kwa kuwa Mungu amewakumbuka. Waliondoka kwako kwa miguu, wakikokotwa na adui zao, Lakini Mungu anawarejeza kwako wameinuliwa juu kwa heshima kama katika kiti cha enzi. Maana kwa maagizo ya Mungu kila kilima kirefu kitashushwa, na milima ya milele. Na mabonde yote yatajazwa, hata nchi iwe sawa, Ili Israeli aende salama katika utukufu wa Mungu. Nayo misitu, na miti yote itoayo harufu nzuri, Imemtia Israeli kivuli kwa amri ya Mungu; Kwa kuwa Mungu atamwongoza Israeli kwa furaha katika mwangaza wa utukufu wake, kwa ile rehema na haki itokayo kwake.

Wimbo wa Katikati

Zab 126:1-6

Bwana alipowarejeza mateka wa Sayuni,
Tulikuwa kama waotao ndoto.
Ndipo kinywa chetu kilipojaa kicheko,
Na ulimi wetu kelele za furaha.
(K) Bwana alitutendea mambo makuu, tulikuwa tukifurahi.

Ndipo waliposema katika mataifa,
Bwana amewatendea mambo makuu,
Bwana alitutendea mambo makuu,
Tulikuwa tukifurahi.
(K) Bwana alitutendea mambo makuu, tulikuwa tukifurahi.

Ee Bwana, uwarejeze watu wetu waliofungwa,
Kama vijito vya Kusini,
Wapandao kwa machozi,
Watavuna kwa kelele za furaha.
(K) Bwana alitutendea mambo makuu, tulikuwa tukifurahi.

Ingawa mtu anakwenda zake akilia,
Azichukuapo mbegu za kupanda,
Hakika atarudi kwa kelele za furaha,
Aichukuapo miganda yake.
(K) Bwana alitutendea mambo makuu, tulikuwa tukifurahi.

Somo la 2

Flp 1:3-6,8-11

Ndugu zangu: Namshukuru Mungu wangu kila wakati niwakumbukapo, siku zote kila niwaombeapo ninyi nyote nikisema sala zangu kwa furaha kwa sababu ya ushirika wenu katika kuieneza Injili tangu siku ile ya kwanza hata leo hivi. Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema miongoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu. Maana Mungu ni shahidi wangu, jinsi ninavyowaonea shauku ninyi nyote katika moyo wake Kristo Yesu. Na hii ndiyo dua yangu, kwamba pendo lenu lizidi kuwa jingi sana, katika hekima na ufahamu wote; mpate kuyakubali yaliyo mema; ili mpate kuyakubali yaliyo mema; ili mpate kuwa na mioyo safi, bila kosa, mpaka siku ya Kristo; hali mmejazwa matunda ya haki, kwa njia ya Yesu Kristo, kwa utukufu na sifa ya Mungu.

Shangilio

Lk 3:4-6

Aleluya, aleluya,
Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake.
Aleluya.

Injili

Lk 3:1-6

Mwaka wa kumi na tano wa kutawala kwake Kaisari Tiberio, Pontio Pilato alipokuwa liwali wa Uyahudi, na Herode mfalme wa Galilaya, na Filipo, ndugu yake mfalme wa Iturea na nchi ya Trakoniti, na Lisania mfalme wa Abilene, wakati wa ukuhani mkuu wa Anasi na Kayafa, neno la Mungu lilimfikia Yohane, mwana wa Zakaria, jangwani. Akafika nchi yote iliyo karibu na Yordani, akihubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi, kama ilivyoandikwa katika chuo cha maneno ya nabii Isaya: Sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, yanyosheni mapito yake. Kila bonde litajazwa, Na kila mlima na kilima kitashushwa; Palipopotoka patakuwa pamenyoka, Na palipoparuza patalainishwa; Na wote wenye mwili watauona wokovu wa Mungu.

Maoni


Ingia utoe maoni