Masomo ya Misa
Jumamosi ya 33 ya Mwaka (Jumamosi, Novemba 20, 2021)
1Mak 6:1:13
Mfalme Antioko alipokuwa akisafiri katika nchi za juu alisikia habari za Elimaisi, mji wa Uajemi, uliosifiwa sana kwa utajiri wake, fedha yake na dhahabu yake. Hekalu lake lilikuwa na mali nyingi, na humo mlikuwa na ngao za dhahabu, na dirii, na silaha za vita ambazo ziliwekwa humo na Iskanda, mwana wa Filipo, mfalme wa Makedonia aliyekuwa wa kwanza kuwatawala Wayunani. Basi, alifika huko, akitaka kuutwaa mji na kuuteka nyara. Lakini haikuwezekana, kwa sababu shauri lake lilijulikana kwa watu wa mjini, wakajipanga kufanya vita naye. Akakimbia, akaondoka kwa moyo mzito kurudi Babeli. Akaletewa habari huko Uajemi ya kuwa majeshi waliokwenda kuipiga nchi ya Uyahudi wameshindwa; tena Lisia, aliyekwenda kwao na jeshi la nguvu sana, alikimbizwa mbele yao; nao wamepata nguvu nyingi kwa sababu ya silaha na zana za vita na nyara walizoziteka kwa majeshi waliyoyashinda. Zaidi ya hayo, wamelibomoa lile chukizo alilolijengesha juu ya madhabahu Yerusalemu, na kupazungusha patakatifu kuta ndefu, kama zamani, na mji wake Bethsura pia. Ikawa, mfalme alipoyasikia maneno hayo, alishikwa na bumbuazi akafadhaika mno. Akakaa huko siku nyingi, maana alilemewa na huzuni nyingi hata alidhani atakufa. Akawaita rafiki zake wote, akawaambia, Usingizi umefarakana na macho yangu, hata moyo wangu umevunjika kwa taabu. Nasema ndani yangu, Jinsi nilivyosibiwa! Ninazama katika maji mengi! Katika enzi yangu nalikuwa mstahiki, mwenye kupendwa. Lakini sasa nayakumbuka mabaya niliyoyafanya Yerusalemu, jinsi nilivyovichukua vyombo vyote vya fedha na dhahabu vilivyokuwapo, na kupeleka majeshi kuwaharibu wenyeji wa Yerusalemu bila sababu. Nafahamu ya kuwa kwa sababu hiyo maovu haya yamenipata, hata, tazama, ninakufa kihoro katika nchi ya kigeni.
Zab 9:1-2,5,15,18
Nitamshukuru Bwana kwa moyo wangu wote;
Nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu;
Nitafurahi na kukushangilia Wewe;
Nitaliimbia jina lako, Wewe Uliye juu.
(K) Nitaufurahia wokovu wako, Ee Bwana.
Kwa sababu adui zangu hurudi nyuma;
Hujikwaa na kuangamia mbele zako.
Umewakembea mataifa;
Na kumwangamiza mdhalimu;
Umelifuta jina lao milele na milele.
(K) Nitaufurahia wokovu wako, Ee Bwana.
Mataifa wamezama katika shimo walilolifanya;
Kwa wavu waliouficha imenaswa miguu yao.
Kwa maana mhitaji hatasahauliwa daima;
Matumaini ya wanyonge hayatapotea milele.
(K) Nitaufurahia wokovu wako, Ee Bwana.
Efe 1:17,18
Aleluya, aleluya,
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristu, awape roho ya hekima mjue tumaini la mwito wake.
Aleluya.
Lk 20:27-40
Baadhi ya masadukayo, wale wasemao ya kwamba hakuna ufufuo, walimwendea Yesu, wakamwuliza, wakisema, Mwalimu, Musa alituandikia ya kuwa, mtu akifiwa na dnugu yake mwenye mke, lakini hana mtoto, na amtwae huyu mke, ampatie ndugu yake mzao. Basi, kulikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa mke, akafa hana mtoto; na wa pili akamtwaa yule mke, akafa hana mtoto; hata wa tatu akamwoa, na kadhalika wote saba, wakafa, wasiache watoto. Mwisho akafa yule mke naye. Basi, katika ufufuo atakuwa mke wa yupi? Maana aliolewa na wote saba. Yesu akawaambia, Wana wa ulimwengu huu huoa na kuolewa; lakini, wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi; wala hawawezi kufa tena; kwa sababu huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu, kwa vile walivyo wana wa ufufuo. Lakini, ya kuwa wafu hufufuliwa, hata na Musa alionyesha katika sura ya Kijiti, hapo alipomtaja Bwana kuwa ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Naye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai; kwa kuwa wote huishi kwake. Waandishi wengine wakajibu wakamwambia, Mwalimu, umesema vema; wala hawakuthubutu kumwuliza neno baada ya hayo.
Maoni
Ingia utoe maoni