Jumanne. 26 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Kumbukumbu ya Waamini Marehemu wote (Jumanne, Novemba 02, 2021)  

Somo la 1

Hek 3:1-9

Roho zao wenye haki wamo mkononi mwa Mungu, wala maumivu hayatawagusa. Machoni pa watu walio wajinga walionekana kwamba wamekufa, na kufariki kwao kulidhaniwa kuwa ni hasara yao, na kusafiri kwao kutoka kwetu kuwa ni uharibifu wao; bali wao wenyewe wamo katika amani. Kwa sababu hata ikiwa (waonavyo watu) wanaadhibiwa, hata hivyo taraja lao limejaa kutokufa na wakiisha kustahimili kurudiwa kidogo watapokea wingi wa mema. Kwa kuwa Mungu amewajaribu na kuwaona kuwa wamestahili, kama dhahabu katika tanuru aliwajaribu, akawakubali mithili ya kafara. Wakati wa kujiliwa kwao watang'aa, na kama vimulimuli katika mabua makavu watametameta. Watawahukumu mataifa na kuwatawala kabila za watu; naye Bwana atawamiliki milele na milele. Wenye kumtumaini watafahamu yaliyo kweli na waaminifu watakaa naye katika upendo; mradi neema na rehema zina wateule wake

Wimbo wa Katikati

Zab. 23

Bwana ndiye mchungaji wangu,
Sitapungukiwa na kitu.
Katika malisho ya majani mabichi hunilaza.
Kando ya maji ya utulivu huniongoza.
(K)Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu

Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza,
Katika njia za haki kwa ajili ya jjina lake.
Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti,
Sitaogopa mabaya;
Kwa maana wewe upo pamoja nami,
Gongo lako na fimbo yangu vyanifariji.
(K)Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu

Waandaa meza mbele yangu,
Machoni pa watesi wangu.
Umenipaka mafuta kichwani pangu,
Na kikombe changu kinafurika.
(K)Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu

Hakika wema na fadhili zitanifuata,
Siku zote za maisha yangu;
Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele.
(K)Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu

Somo la 2

Rum 6:3-9

Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake? Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima. Kwa maana kama mlivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika mtaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake; mkijua neno hili, ya kuwa utu wetu wa kale ulisulibishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena;

Shangilio

Ufu. 14:13

Aleluya, aleluya,
Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa! Wapate kupumzika baada ya taabu zao, kwa kuwa matendo yao yafuatana nao.
Aleluya.

Injili

Yn 6:37-40

Yesu aliwaambia mkutano: wote anipao Baba watakuja kwangu; wala ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe. Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka. Na mapenzi yake aliyenipeleka ni haya, ya kwamba katika wote alionipa nisimpoteze hata mmoja, bali nimfufue siku ya mwisho. Kwa kuwa mapenzi yake Baba yangu ni haya, ya kwamba kila amtazamaye Mwana na kumwamini yeye, awe na uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.

Maoni

Betram Mushi

Milele....Amina...Tumshukuru..Mungu.

Ingia utoe maoni