Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Alhamisi ya 20 ya Mwaka (Alhamisi, Agosti 18, 2016)  

Somo la 1

Eze 36:23-28

Neno la Bwana lilinijia hivi: nitalitakasa jina langu kuu, lililotiwa unajisi katika mataifa, mlilolitia unajisi kati yao; nao mataifa watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, asema Bwana MUNGU, nitakapotakaswa kati yenu mbele ya macho yao. Maana nitawatwaa kati ya mataifa, nami nitawakusanya na kuwatoa katika nchi zote, na kuwarudisha katika nchi yenu wenyewe. Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda. Nanyi mtakaa katika nchi ile niliyowapa baba zenu, nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.

Wimbo wa Katikati

Zab 51:10-13, 16-17

Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu
Usinitenge na uso wako, Wala roho yako mtakatifu usiniondolee.
(K) Nitawanyunyizia maji safi; Nanyi mtakuwa safi, nitawatakaseni na uchafu wenu wote.

Unirudishie furaha ya wokovu wako; Unitegemeze kwa roho ya wepesi.
Nitawafundisha wakosaji njia zako, Na wenye dhambi watarejea kwako.
(K) Nitawanyunyizia maji safi; Nanyi mtakuwa safi, nitawatakaseni na uchafu wenu wote.

Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa, Wewe huridhii sadaka ya kuteketezwa.
Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika; Moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu, hutaudharau.
(K) Nitawanyunyizia maji safi; Nanyi mtakuwa safi, nitawatakaseni na uchafu wenu wote.

Shangilio

Zab 95:8

Aleluya, aleluya
Ikiwa leo mwaisikia sauti yake, Msifanye migumu mioyo yenu;
Aleluya

Injili

Mt 22:1-14

Yesu aliwaambia makuhani na makutano kwa mithali, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyemfanyia mwanawe arusi. Akawatuma watumwa wake wawaite walioalikwa kuja arusini; nao wakakataa kuja. Akatuma tena watu kwa wengine, akisema, Waambieni wale walioalikwa, Tazameni, nimeandaa karamu yangu; ng'ombe zangu na vinono vimekwisha kuchinjwa, na vyote vimekuwa tayari, njoni arusini. Lakini hawakujali, wakaenda zao, mmoja shambani kwake, mmoja kwenye biashara yake; nao waliosalia wakawakamata watumwa wake, wakawatenda jeuri, na kuwaua. Basi yule mfalme akaghadhibika; akapeleka majeshi yake, akawaangamiza wauaji wale, akauteketeza mji wao. Kisha akawaambia watumwa wake, Arusi i tayari, lakini wale walioalikwa hawakustahili. Basi enendeni hata njia panda za barabara, na wote mwaonao waiteni arusini. Watumwa wale wakatoka wakaenda njia kuu, wakakusanya wote waliowaona, waovu kwa wema; arusi ikajaa wageni. Lakini alipoingia yule mfalme ili kuwatazama wageni wake, akaona mle mtu mmoja asiyevaa vazi la arusi.Akamwambia, Rafiki, uliingiaje humu nawe huna vazi la arusi? Naye akatekewa. Mfalme akawaambia watumishi, Mfungeni mikono na miguu, mchukueni mkamtupe katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache.

Maoni


Ingia utoe maoni