Masomo ya Misa
Dominika ya 27 ya Mwaka (Jumapili, Oktoba 03, 2021)
Mwa 2:18:24
Bwana Mungu alisema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanya msaidizi wa kufanana naye. Bwana Mungu akafanyiza kutoka katika ardhi kila mnyama wa msituni, na kila ndege wa angani, akamletea Adamu ilia one atawaitaje; kila kiumbe hai, jna alilokiita Adamu likawa ndilo jina lake. Adamu akawapa majina yao kila mnyama wa kufugwa, na ndege wa angani, na kila mnyama wa mwituni; lakini hakuonekana wa kumsaidia Adamu aliyefanana naye. Bwana Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake, na ule ubavu alioutwaa katika Adamu Bwana Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu. Adamu akasema, Sasa huyo ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume. Kwa hiyo mwanamume, atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.
Zab 128
Heri kila mtu amchaye Bwana,
Aendaye katika njia yake.
Taabu ya mikono yako hakika utaila,
Utakuwa mwenye heri na baraka tele.
(K) Bwana atubariki siku zote za maisha yetu.
Mke wako atakuwa kama mzabibu uzaao,
Vyumbani mwa nyumba yako.
Wanao kama miche ya mizeituni,
Wakizunguka meza yako.
(K) Bwana atubariki siku zote za maisha yetu.
Hakika, atabarikiwa hivyo,
Yule amchaye Bwana.
Bwana akubariki toka Sayuni,
Uone uheri wa Yerusalemu siku zote za maisha yako;
Naam, ukawaone wana wa wanao.
Amani ikae na Israeli.
(K) Bwana atubariki siku zote za maisha yetu.
Ebr 2:9-11
Ndugu, twamwona yeye aliyefanywa mdogo punde kuliko malaika, yaani, Yesu, kwa sababu ya maumivu ya mauti, amevitwa taji ya utukufu na heshima, ili kwa neema ya Mungu aionje mauti kwa ajili ya kila mtu. Kwa kuwa ilimpasa yeye, ambaye kwa ajili yake na kwa njia yake vitu vyote vimekuwapo, akileta wana wengi waufikilie utukufu, kumkamilisha kiongozi mkuu wa wokovu wao kwa njia ya mateso. Maana yeye atakassaye na hao wanaotakaswa wote pia watoka kwa mmoja. Kwa ajili hii haoni haya kuwaita ndugu zake.
Yn 14:23
Aleluya, aleluya!
Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake.
Aleluya.
Mk 10:2-16
Mafarisayo walimwendea Yesu, wakamwuliza, Je, ni halali mtu kumwacha mkewe? Huku wakimjaribu. Naye akajibu, akawaambia, Musa aliwaamuru nini? Wakasema, Musa alitoa ruhusa kuandika hati ya talaka na kumwacha. Yesu akawaambia, Kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu aliwaandikia amri hii. Lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja, hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe. Hata nyumbani tena wanafunzi wakamwuliza habari ya neno hilo. Akawaambia, Kila mtu atakayemwacha mkewe na kuoa mwingine azini juu yake; na mke, akimwacha mumewe na kuolewa na mtu mwingine azini. Basi wakamletea watoto wadogo ili awaguse; wanafunzi wake wakawakemea. Ila Yesu alipoona alichukizwa sana, akawaambia, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao. Amin, nawaambieni, Yeyote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa. Akawakumbatia, akaweka mikono juu yao, akawabarikia.
Maoni
Johanes Ishengoma
Ahsant kwa nenoSeverin Josephat
Amina mungu awabariki kwa kusaidia watu ambao hawajaenda Kanisani kufikiwa na masomo ya j2Jonas Tarimo
AminaBetram Mushi
Milele....Amina...tumshukuru..Mungu.Ingia utoe maoni