Masomo ya Misa
Jumatano ya 20 Mwaka (Jumatano, Agosti 17, 2016)
Eze 34:1-11
Neno la Bwana likanijia, kusema, Mwanadamu, toa unabii juu ya wachungaji wa Israeli, toa unabii, uwaambie, naam, hao wachungaji, Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao wachungaji wa Israeli, wanaojilisha wenyewe; je! Haiwapasi wachungaji kuwalisha kondoo? Mnawala walionona, mnajivika manyoya, mnawachinja walionona; lakini hamwalishi kondoo. Wagonjwa hamkuwatia nguvu, wala hamkuwaponya wenye maradhi, wala hamkuwafunga waliovunjika, wala hamkuwarudisha waliofukuzwa, wala hamkuwatafuta waliopotea; bali kwa nguvu na kwa ukali mmewatawala. Nao wakatawanyika, kwa sababu hapakuwa na mchungaji; wakawa chakula cha wanyama- mwitu, wakatawanyika. Kondoo zangu walitanga-tanga katika milima yote, na juu ya kila kilima kirefu; naam, kondoo zangu walitawanyika juu ya uso wote wa dunia; wala hapakuwa na mtu aliyewaulizia, wala kuwatafuta. Basi, enyi wachungaji, lisikieni neno la Bwana; Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, kwa sababu kondoo zangu walikuwa mateka, kondoo zangu wakawa chakula cha wanyama-mwitu wote, kwa sababu hapakuwa na mchungaji, wala wachungaji wangu hawakutafuta kondoo zangu, bali wachungaji walijilisha wenyewe wala hawakuwalisha kondoo zangu; kwa sababu hiyo, enyi wachungaji, lisikieni neno la Bwana; Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu ya wachungaji; nami nitawataka kondoo zangu mikononi mwao, nami nitawaachisha hiyo kazi ya kuwalisha kondoo; nao wachungaji hawatajilisha wenyewe tena; nami nitawaokoa kondoo zangu vinywani mwao, wasiwe tena chakula chao. Maana, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi mwenyewe, naam, mimi, nitawatafuta kondoo zangu, na kuwaulizia.
Zab 23:1-6
Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu.
Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, Kando ya maji ya utulivu huniongoza.
Hunihuisha nafsi yangu;
(K) Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu
Huniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya;
Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji.
(K) Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu
Waandaa meza mbele yangu, Machoni pa watesi wangu.
Umenipaka mafuta kichwani pangu, Na kikombe changu kinafurika.
(K) Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu
Hakika wema na fadhili zitanifuata Siku zote za maisha yangu;
Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele.
(K) Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu
Ebr 4:12
Aleluya, aleluya
Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
Aleluya
Mt 20:1-16
Yesu aliwaambia wafuasi wake: Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu mwenye nyumba aliyetoka alfajiri kwenda kuajiri wakulima awapeleke katika shamba lake la mizabibu. Naye alipokwisha kupatana na wakulima kuwapa kutwa dinari, aliwapeleka katika shamba lake la mizabibu. Akatoka mnamo saa tatu, akaona wengine wamesimama sokoni wasiokuwa na kazi;na hao nao akawaambia, Enendeni nanyi katika shamba langu la mizabibu, na iliyo haki nitawapa. Wakaenda. Akatoka tena mnamo saa sita na saa kenda, akafanya vile vile. Hata kama saa kumi na moja akatoka, akakuta wengine wamesimama, akawaambia, Mbona mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi? Wakamwambia, Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri. Akawaambia, enendeni nanyi katika shamba la mizabibu. Kulipokuchwa, yule bwana wa shamba akamwambia msimamizi wake, Waite wakulima, uwalipe ujira wao, ukianzia wa mwisho hata wa kwanza. Na walipokuja wale wa saa kumi na moja, walipokea kila mtu dinari. Na wale wa kwanza walipokuja, walidhani kwamba watapokea zaidi; na hao pia wakapokea kila mtu dinari. Basi wakiisha kuipokea, wakamnung'unikia mwenye nyumba, wakisema, Hao wa mwisho wametenda kazi saa moja tu, nawe umewasawazisha na sisi tuliostahimili taabu na hari za mchana kutwa. Naye akamjibu mmoja wao, akamwambia, Rafiki, sikudhulumu; hukupatana nami kwa dinari? Chukua iliyo yako, uende zako; napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe. Si halali yangu kutumia vilivyo vyangu kama nipendavyo? Au jicho lako limekuwa ovu kwa sababu ya mimi kuwa mwema? Vivyo hivyo wa mwisho watakuwa wa kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho.
Maoni
Ingia utoe maoni