Masomo ya Misa
Ijumaa ya 20 ya Mwaka (Ijumaa, Agosti 20, 2021)
Rut 1:1,3-6, 14-16, 22
Ikawa zamani za Waamuzi walipoamua, kulikuwa na njaa katika nchi. Akaondoka mtu mmoja wa Bethlehemu ya Yuda, akaenda kukaa katika nchi ya Moabu, yeye na mkewe na wanawe wawili. Akafa Elimeleki, mumewe Naomi; na yule mwanamke akasalia na wanawe wawili. Nao wakaoa wake katika wanawake wa Moabu; na jina la mmoja aliitwa Orpa, na jina la wa pili Ruthuu. Wakakaa huko yapata miaka kumi. Wakafa na Maloni na Kilioni wote wawili; na huyo mwanamke akawa amefiwa na wanawe wawili, na mumewe pia. Ndipo alipoondoka, yeye na wakweze, ili kurudi kutoka nchi ya Moabu; maana huko katika nchi ya Moabu amesikia ya kwamba Bwana amewajilia watu wake na kuwapa chakula. Nao wakapaza sauti zao, wakalia tena, na Orpa akambusu mkwewe, lakini Ruthuu akaambatana naye. Naye akasema, Tazama, shemeji yako amerejea kwa watu wake, na kwa mungu wake; basi urejee wewe umfuate shemeji yako. Naye Ruthuu akasema, Usinisihi nikuache, Nirejee nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu; Basi Naomi akarudi; pamoja na Ruthuu Mmoabi, mkwewe; ambao walirudi kutoka nchi ya Moabu; nao wakafika Bethlehemu mwanzo wa mavuno ya shayiri.
Zab 146:5-10
Heri ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake,
Na tumaini lake ni kwa Bwana, Mungu wake,
Aliyezifanya mbingu na nchi,
Bahari na vitu vyote vilivyomo.
(K) Ee nafsi yangu, umsifu Bwana.
Huishika kweli milele,
Huwafanyia hukumu walioonewa,
Huwapa wenye njaa chakula;
Bwana hufungua waliofungwa;
(K) Ee nafsi yangu, umsifu Bwana.
Bwana huwafumbua macho waliopofuka;
Bwana huwainua walioinama;
Bwana huwapenda wenye haki;
Bwana huwahifadhi wageni;
(K) Ee nafsi yangu, umsifu Bwana.
Huwategemeza yatima na mjane;
Bali njia ya wasio haki huipotosha.
Bwana atamiliki milele, Mungu wako,
Ee Sayuni, kizazi hata kizazi. Haleluya.
(K) Ee nafsi yangu, umsifu Bwana.
Mt 22:34-40
Mafarisayo waliposikia ya kwamba amewafumba kinywa wale Masadukayo, walifanya shauri pamoja.Mmoja wao, mwana-sheria, akamwuliza, akimjaribu; Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu? Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii.
Maoni
Florence Nduku
Mungu awabariki kwa neno na injili ya leo inayo tufundisha jinsi ya kuishi tukipendanaIngia utoe maoni