Masomo ya Misa
Jumamosi ya 15 ya Mwaka (Jumamosi, Julai 17, 2021)
Kut 12:37-42
Wana wa Israeli walisafiri kutoka Ramesesi mpaka Sukothi, walipata hesabu yao kama watu sita mia elfu watu waume waliokwenda kwa miguu, bila kuhesabu watoto. Na kundi kubwa la watu waliochangamana mno wakakwea pamoja nao; na kondoo na ng'ombe, wanyama wengi sana. Nao wakaoka mikate isiyochachwa ya ule unga waliouchukua walipotoka Misri, maana, haukutiwa chachu, kwa sababu walitolewa watoke Misri, wasiweze kukawia, nao walikuwa hawajajifanyia tayari chakula. Basi wana wa Israeli kukaa kwao, maana, muda waliokaa ndani ya Misri, ulikuwa ni miaka mia nne na thelathini. Ilikuwa mwisho wa miaka hiyo mia nne na thelathini, ilikuwa siku ile ile, ya kwamba majeshi yote ya Bwana yalitoka nchi ya Misri. Ni usiku wa kuangaliwa sana mbele za Bwana kwa sababu ya kuwatoa katika nchi ya Misri; huu ndio usiku wa Bwana, ambao wapasa kuangaliwa sana na wana wa Israeli wote katika vizazi vyao.
Zab 136:1, 10-15, 23-24
Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema;
Kwa maana fadhili zake ni za milele.
Yeye aliyewapiga Wamisri kwa kuwaua wazaliwa wa kwanza wao;
Kwa maana fadhili zake ni za milele.
Akawatoa Waisraeli katikati yao;
Kwa maana fadhili zake ni za milele.
(K) Fadhili zake ni za milele.
Kwa mkono hodari na mkono ulionyoshwa;
Kwa maana fadhili zake ni za milele.
Yeye aliyeigawa Bahari ya Shamu;
Kwa maana fadhili zake ni za milele.
Akawavusha Israeli katikati yake;
Kwa maana fadhili zake ni za milele.
(K) Fadhili zake ni za milele.
Aliyetukumbuka katika unyonge wetu;
Kwa maana fadhili zake ni za milele.
Akatuokoa na watesi wetu;
Kwa maana fadhili zake ni za milele.
(K) Fadhili zake ni za milele.
Mt 12:14-21
Mafarisayo walitoka wakafanya shauri juu ya Yesu jinsi ya kumwangamiza. Naye Yesu hali akiyafahamu hayo akaondoka huko; na watu wengi wakamfuata; akawaponya wote, akawakataza wasimdhihirishe; ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Tazama, mtumishi wangu niliyemteua; mpendwa wangu, moyo wangu uliyependezwa naye; nitatia roho yangu juu yake, naye atawatangazia Mataifa hukumu. Hatateta wala hatapaza sauti yake; wala mtu hatasikia sauti yake njiani. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima, hata ailetapo hukumu ikashinda. Na jina lake Mataifa watalitumainia.
Maoni
Ingia utoe maoni