Jumanne. 26 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Kumbukumbu ya Moyo Safi wa Bikira Maria Imakulata (Jumamosi, Juni 12, 2021)  

Somo la 1

Isa. 61:9-11

Kizazi chao kitajulikana katika mataifa, na uzao wao katika kabila za watu; wote wawaonao watakiri ya kuwa wao ni kazazi kilichobarikiwa na Bwana. Nitafurahi sana katika bwana, nafsi yangu itashangilia katika Mungu wangu; maana amenivika mavazi ya wokovu, amenifunika vazi la haki, kama bwana rusi ajipambavyo kwa kilemba cha maua, na kama bibi harusi ajipambavyo kwa vyombo vya dhahabu. Maana kama nchi itoavyo machipuko yake, na kama bustani ioteshavyo vitu vilivyopandwa ndani yake; ndivyo Bwana Mungu atakavyootesha haki na sifa mbele ya mataifa yote.

Wimbo wa Katikati

1 Sam. 2:1, 4-8

Moyo wangu wamshangilia Bwana,
Pembe yangu imetukuka katika Bwana,
Kinywa change kimepanuka juu ya adui zangu;
Kwa kuwa naufurahia wokovu wako.
(K) Moyo wangu wamshangilia Bwana.

Pinde zao mashujaa zimevunjika,
Na hao waliojikwaa wamefungiwa nguvu.
Walioshiba wamejikodisha ili kupata chakula,
Na hao waliokuwa na njaa wamepata raha.
Naam, huyo aliyekuwa tasa amezaa watoto saba,
Na yeye aliye na wana wengi amedhoofika.
(K) Moyo wangu wamshangilia Bwana.

Bwana huua, naye hufanya kuwa hai;
Hushusha hata kuzimu, tena huleta juu.
Bwana hufukarisha mtu, naye hutajirisha;
Hushusha chini, tena huinua juu.
(K) Moyo wangu wamshangilia Bwana.

Humwinua mnyonge kutoka mavumbini,
Humpandisha mhitaji kutoka jaani,
Ili awaketishe pamoja na wakuu,
Wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu.
(K) Moyo wangu wamshangilia Bwana.

Injili

Lk. 2:41-51

Wazee wa Yesu huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka. Na alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu; na walipokwisha kuzitimiza siku, wakati wa kurudi kwao, yule mtoto Yesu alibaki nyuma huko Yerusalemu, na wazee wake walikuwa hawana habari. Nao wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenenda mwendo wa kutwa, wakawa wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao; na walipomkosa, wakarejea Yerusalemu, huku wakimtafuta. Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake. Na walipomwona walishangaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni. Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu? Nao hawakuelewa na neno hilo alilowaambia. Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake. Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.

Maoni

Douglas Anthony

TYK Somo laleo tunafundishwa turuhusu watoto waweze kujua neno la mungu angali wakiwa watoto. Kama injili ilivyo sema Yesu aliendelea kukuwa kwa kimo na hekima Basi ndivyo hivyo tuwafundishe angali wakiwa wadogo tuwape moyo wakujua nini maana ya ukristo na imani yetu Bila wafundisha angali wadogo ukubwani ningumu kuwa kundini msingi huanzia chini

Ingia utoe maoni