Jumanne. 26 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Sherehe ya Utatu Mtakatifu (Jumapili, Mei 30, 2021)  

Somo la 1

Kum. 4 :32-34, 39-40

Musa aliwaambia makutano: Uliza sasa siku zilizopita, zilizokuwa kabla yako, tangu siku ile Mungu aliyoumba mwanadamu juu ya nchi, na toka pembe hii ya mbingu hata pembe hii, kwamba kumetukia neno lo lote kama hili kubwa, au kwamba kumesikiwa habari ya neno kama hili? Je! watu wakati wo wote wameisikia sauti ya Mungu ikinena toka kati ya moto, kama wewe ulivyosikia, wasife? Au Mungu amekwenda wakati gani akajitwalia taifa toka kati ya taifa lingine, kwa majaribu, na kwa ishara, na kwa maajabu, na kwa vita, na kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa maogofya makuu, kama vile Bwana, Mungu wenu, alivyowatendea ninyi katika Misri, mbele ya macho yenu? Kwa hiyo ujue, leo hivi, ukaweke moyoni mwako, ya kuwa Bwana ndiye Mungu katika mbingu juu, na katika nchi chini; hapana mwingine. Basi, zishike sheria zake, na amri zake, ninazokuamuru leo, upate kufanikiwa, wewe na watoto wako baada yako, na siku zako ziwe nyingi katika nchi ile akupayo Bwana, Mungu wako, milele.

Wimbo wa Katikati

Zab. 33 :4-6, 9, 18-20, 22

Kwa kuwa neno la Bwana ni adili,
Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.
Bwana huzipenda haki na hukumu,
Nchi imejaa fadhili za Bwana.
(K) Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao.

Kwa neno la Bwana mbingu zilifanyika.
Na jeshi lake lote kwa pumzi ya kinywa chake.
Maana Yeye alisema, ikawa;
Na Yeye aliamuru, ikasimama.
(K) Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao.

Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao,
Wazingojeao fadhili zake.
Yeye huwaponya nafsi zao na mauti,
Na kuwahuisha wakati wa njaa.
(K) Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao.

Nafsi zetu zinamngoja Bwana,
Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu.
Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi,
Kama vile tulivyokungoja Wewe.
(K) Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao.

Somo la 2

Rum. 8 :14-17

Kila mtu anaongozwa na Roho wa Mungu, huyo ndio mtoto wa Mungu. Kwa kuwa hamkupokea tena roho ya utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba. Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithi pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.

Shangilio

Ufu 1:8

Aleluya, Aleluya,
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, Mungu ambaye yupo, aliyekuwako, na atakayekuja.
Aleluya.

Injili

Mt. 28: 16-20

Wale wanafunzi kumi na mmoja wakaenda Galilaya mpaka mlima ule aliowaagiza Yesu. Nao walipomwona, walimsujudia; lakini baadhi yao waliona shaka. Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi sikuzote, hata ukamilifu wa dahari.

Maoni


Ingia utoe maoni