Masomo ya Misa
Jumatano ya 8 ya Mwaka (Jumatano, Mei 26, 2021)
Ybs 36:1, 4-5, 10-17
Ee Bwana, Mungu wa watu wote utuokoe; uangalie, uwatishe wataifa yote; uuinue mkono wako juu ya watu wageni. Wakujue wewe kama sisi tukujuavyo, ya kwamba hakuna Mungu ila Wewe peke yako. Tuoneshe ishara tena, na kufanya mambo ya ajabu. uutukuze mkono, naam, mkono wako wa kuume. Uwakusanye kabila zote za Yakobo, na kuwafanya urithi wako kama siku za kale. Ee Bwana, uwarehemu watu walioitwa kwa jina lako, na Israeli uliyemwita mzaliwa wa kwanza kwako. Uuonee huruma mji wa patakatifu pako. Yerusalemu, mahali pako pa raha; uujaze Sioni adhama yako, na patakatifu pako utukufu wako. Uwashuhudie wale waliokuwa viumbe vyako tangu awali, na kuyathibitisha maneno ya unabii yaliyonenwa kwa jina lako. Uwajazi wakungojao, na watu watasadiki manabii wako. Ee Bwana uisikilize sala yao wakuombao, sawasawa na kibali chako kwa watu wako; na wote wakaao duniani watajua ya kwamba Wewe ndiwe Bwana, Mungu wa milele.
Zab 79:8-9, 11, 13
Usikumbuke juu yetu maovu ya baba zetu,
Rehema zako zije kutulaki hima,
Kwa maana tumedhilika sana.
(K) Ee Bwana, Mungu wa watu wote, utuokoe
Ee Mungu wa wokovu wetu, utusaidie,
Kwa ajili ya utukufu wa jina lako.
Utuokoe, utughofiri dhambi zetu, Kwa ajili ya jina lako.
(K) Ee Bwana, Mungu wa watu wote, utuokoe
Na sisi tulio watu wako,
Na kondoo za malisho yako,
Tutakushukuru milele;
Tutazisimulia sifa zako kizazi kwa kizazi.
(K) Ee Bwana, Mungu wa watu wote, utuokoe
Mk 10:32-45
Walikuwako njiani, huku wakipanda kwenda Yerusalemu; na Yesu alikuwa akiwatangulia; wakashangaa, nao katika kufuata wakaogopa. Akawatwaa tena wale Thenashara, akaanza kuwaambia habari za mambo yatakayompata, akisema, Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu; na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa wakuu wa makuhani na waandishi, nao watamhukumu afe, watamtia mikononi mwa Mataifa, nao watamdhihaki, na kumtemea mate, na kumpiga mijeledi, na kumwua; na baada ya siku tatu atafufuka. Na Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, wakamwendea, wakamwambia, Mwalimu, twataka utufanyie lo lote tutakalokuomba. Akawaambia, Mwataka niwafanyie nini? Wakamwambia, Utujalie sisi tuketi, mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika utukufu wako. Yesu akawaambia, Hamjui mnaloliomba. Mwaweza kunywea kikombe ninyweacho mimi, au kubatizwa ubatizo nibatizwao mimi? Wakamwambia, Twaweza. Yesu akawaambia, Kikombe ninyweacho mimi mtakinywea, na ubatizo nibatizwao mimi mtabatizwa; lakini habari ya kuketi mkono wangu wa kuume au mkono wangu wa kushoto si langu kuwapa, ila wao watapewa waliowekewa tayari. Hata wale kumi waliposikia wakaanza kuwakasirikia Yakobo na Yohane. Yesu akawaita, akawaambia, Mwajua ya kuwa wale wanaohesabiwa kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote. Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.
Maoni
Ingia utoe maoni