Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumamosi ya 17 ya Mwaka (Jumamosi, Julai 30, 2016)  

Somo la 1

Yer 26:11-16, 24

Makuhani, na manabii, wakawaambia wakuu na watu wote, wakisema, Mtu huyu amestahili kufa, kwa sababu ametabiri juu ya mji huu, kama mlivyosikia kwa masikio yenu. Ndipo Yeremia akawaambia wakuu wote na watu wote, akisema, Bwana ndiye aliyenituma kutabiri juu ya nyumba hii, na juu ya mji huu, maneno hayo yote mliyoyasikia. Basi sasa, tengenezeni njia zenu, na matendo yenu, mkaisikilize sauti ya Bwana, Mungu wenu; naye Bwana atayaghairi mabaya aliyoyanena juu yenu. Lakini kwangu mimi, tazama, mimi nipo hapa mikononi mwenu; nitendeni myaonayo kuwa mema na haki mbele ya macho yenu. Lakini jueni yakini ya kuwa, mkiniua, mtajiletea juu yenu damu isiyo na hatia itakuwa juu yenu, na juu ya mji huu, na juu ya wenyeji wake; kwa maana ni kweli Bwana amenituma kwenu, kuwaambieni yote mliyoyasikia. Ndipo wakuu na watu wote wakawaambia makuhani, na manabii, wakisema, Mtu huyu hastahili kuuawa; kwa maana amesema nasi katika jina la Bwana Mungu wetu. Lakini mkono wa Ahikamu, mwana wa Shafani, alikuwa pamoja na Yeremia, wasimtie katika mikono ya watu auawe.

Wimbo wa Katikati

Zab 69:14-15, 29-30, 32-33

Uniponye kwa kunitoa matopeni, Wala usiniache nikazama.
Na niponywe nao wanaonichukia, Na katika vilindi vya maji.
Mkondo usinigharikishe, wala vilindi visinimeze,
Wala shimo lisifumbe kinywa chake juu yangu.
(K) Kwa wingi wa fadhili zako, unijibu, Ee Bwana.

Nami niliye maskini na mtu wa huzuni, Mungu, wokovu wako utaniinua.
Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo, Nami nitamtukuza kwa shukrani.
(K) Kwa wingi wa fadhili zako, unijibu, Ee Bwana.

Walioonewa watakapoona watafurahi;
Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe.
Kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji,
Wala hawadharau wafungwa wake.
(K) Kwa wingi wa fadhili zako, unijibu, Ee Bwana.

Shangilio

Mt 5:10

Aleluya, aleluya
Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.
Aleluya

Injili

Mt 14:1-12

Wakati ule mfalme Herode alisikia habari za Yesu, akawaambia watumishi wake, Huyo ndiye Yohana Mbatizaji; amefufuka katika wafu; na kwa hiyo nguvu hizo zinatenda kazi ndani yake. Maana Herode alikuwa amemkamata Yohana, akamfunga, akamtia gerezani, kwa ajili ya Herodia, mke wa Filipo nduguye. Kwa sababu Yohana alimwambia, Si halali kwako kuwa naye. Naye alipotaka kumwua, aliwaogopa watu, maana walimwona Yohana kuwa nabii. Hata ilipofika sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti Herodia alicheza mbele ya watu, akampendeza Herode. Hata akaahidi kwa kiapo ya kwamba atampa lo lote atakaloliomba. Naye, huku akichochewa na mamaye, akasema, Nipe hapa katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji. Naye mfalme akasikitika; lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya wale walioketi chakulani pamoja naye, akaamuru apewe; akatuma mtu, akamkata kichwa Yohana mle gerezani. Kichwa chake kikaletwa katika kombe, akapewa yule kijana; akakichukua kwa mamaye. Wanafunzi wake wakaenda, wakamchukua yule maiti, wakamzika; kisha wakaenda wakampasha Yesu habari.

Maoni


Ingia utoe maoni