Masomo ya Misa
JUMANNE YA 5 MWAKA (Jumanne, Februari 09, 2016)
1 Fal. 8:22-23, 27-30
Sulemani alisimama mbele ya madhabahu ya Bwana, machoni pa mkutano wote wa Israeli, akaikunjua mikono yake mbinguni. Akasema, Ee Bwana, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe, mbinguni juu wala duniani chini; ushikaye maagano na rehema kwa watumishi wako, waendao mbele zako kwa mioyo yao yote. Lakini Mungu je! Atakaa kweli kweli juu ya nchi? Tazama, mbingu hazikutoshi, wala mbingu za mbingu; sembuse nyumba hii niliyoijenga? Walakini uyaelekee maombi ya mtumwa wako, na dua yake, Ee Bwana, Mungu wangu, uisikilize sauti na maombi ya mtumwa wako, aombayo mbele zako leo. Macho yako yafumbuke na kuielekea nyumba hii usiku na mchana, mahali hapa ulipopataja, ukasema, Hapa ndipo litakapokuwapo jina langu; ili uyasikie maombi ya mtumwa wako aombapo, akikabili mahali hapa. Uisikie dua ya mtumwa wako, na ya watu wako Israeli, watakapoomba wakikabili mahali hapa; naam, sikia huko mbinguni, makao yako; nawe usikiapo, samehe.
Zab. 84:2-4, 9-10 (K) 1
(K) Maskani zako zapendeza kama nini, ee Bwana wa majeshi.
Nafsi yangu imezionea shauku nyua za Bwana,
Naam, na kuzikondea.
Moyo wangu na mwili wangu
Vinamlilia Mungu aliye hai. (K)
Shomoro naye ameona nyumba,
Na mbayuwayu amejipatia kiota,
Alipoweka makinda yake:
Kwenye madhabahu zako, ee Bwana wa majeshi,
Mfalme wangu na Mungu wangu. (K)
Heri wakao nyumbani mwako,
Wanakuhimidi daima.
Ee Mungu, ngao yetu, uangalie,
Umtazame uso masihi wako. (K)
Hakika siku moja katika nyua zako
Ni bora kuliko siku elfu.
Ningependa kuwa bawabu
Nyumbani mwa Mungu wangu,
Kuliko kukaa katika hema za uovu. (K)
Mk. 7:1-13
Mafarisayo, na badhi ya waandishi waliotoka Yerusalemu, wakakusanyika mbele ya Yesu, wakaona wengine katika wanafunzi wake wakila vyakula kwa mikono najisi, yaani, isiyonawiwa. Kwa maana Mafarisayo na Wayahudi wote wasiponawa mikono mpaka kiwiko, hawali, wakishika mapokeo ya wazee wao; tena wakitoka sokoni, wasipotawadha, hawali; na yako mambo mengine waliyopokea kuyashika, kama kuosha vikombe, na midumu, na vyombo vya shaba. Basi wale Mafarisayo na waandishi wakamwuliza, Mbona wanafunzi wako hawaendi kwa kuyafuata mapokeo ya wazee, bali hula chakula kwa mikono najisi? Akawambia, Isaya alitabiri vema juu yenu ninyi wanafiki, kama ilivyoandikwa, Watu hawa huniheshimu kwa midomo, ila mioyo yao iko mbali nami; Nao waniabudu bure, wakifundisha mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu. Ninyi mwaiacha amri ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya wanadamu. Akawaambia, Vema? Mwaikataa amri ya Mungu mpate kuyashika mapokeo yenu. Maana Musa alisema, Waheshimu baba yako na mama yako, na, amtukanaye babaye au mamaye kufa na afe. Bali ninyi husema, Mtu akimwambia babaye au mamaye. Ni Korbani, yaani, wakfu, kitu changu chochote kikupasacho kufaidiwa nacho, huwa basi; wala hammruhusu baada ya hayo kumtendea neno babaye au mamaye; huku mkilitangua neno la Mungu kwa mapokeo yenu mliyopokeana; tena mwafanya mambo mengi yaliyo sawasawa na hayo.
Maoni
Ingia utoe maoni