Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Sikukuu ya Mt. Marta (Ijumaa, Julai 29, 2016)  

Somo la 1

Yer 26:1-9

Mwanzo wa kumiliki kwake Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, neno hili lilitoka kwa Bwana, kusema, Bwana asema hivi, Simama katika uwanja wa nyumba ya Bwana, useme na miji yote ya Yuda, wajao ili kuabudu katika nyumba ya Bwana; sema nao maneno yote ninayokuamuru kuwaambia, usizuie hata neno moja. Labda watasikia, na kughairi na kuacha kila mtu njia yake mbaya; ili niyaghairi mabaya niliyokusudia kuwatenda, kwa sababu ya uovu wa matendo yao. Nawe utawaambia, Bwana asema hivi, Kama hamtaki kunisikia, kwenda katika sheria yangu, niliyoiweka mbele yenu, kuyasikiliza maneno ya watumishi wangu, manabii, ninaowatuma kwenu, naam, nikiondoka mapema na kuwatuma; lakini ninyi hamkuwasikiliza; basi, nitafanya nyumba hii kuwa kama Shilo, na mji huu nitaufanya kuwa laana kwa taifa zote za dunia. Na makuhani, na manabii, na watu wote, wakamsikia Yeremia, hapo aliposema maneno haya katika nyumba ya Bwana. Ikawa, Yeremia alipokuwa amekwisha kusema maneno yote Bwana aliyomwamuru kuwaambia watu wote, ndipo hao makuhani, na manabii, na watu wote, wakamkamata, wakisema, Bila shaka utakufa. Kwa nini umetabiri kwa jina la Bwana, ukisema, Nyumba hii itakuwa kama Shilo, na mji huu utakuwa ukiwa, hautakaliwa na mtu? Watu wote wakamkusanyikia Yeremia katika nyumba ya Bwana.

Wimbo wa Katikati

Zab 69:4, 7-9,13

Wanaonichukia bure ni wengi Kuliko nywele za kichwa changu.
Watakao kunikatilia mbali wamekuwa hodari,
Adui zangu kwa sababu isiyo kweli.
Hata mimi nalilipishwa kwa nguvu Vitu nisivyovichukua.
(K) Kwa wingi wa fadhili zako unijibu, ee Bwana.

Maana kwa ajili yako nimestahimili laumu, Fedheha imenifunika uso wangu.
Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu, Na msikwao kwa wana wa mama yangu.
Maana wivu wa nyumba yako umenila, Na laumu zao wanaokulaumu zimenipata.
(K) Kwa wingi wa fadhili zako unijibu, ee Bwana.

Nami maombi yangu nakuomba Wewe, Bwana, Wakati ukupendezao;
Ee Mungu, Kwa wingi wa fadhili zako unijibu, Katika kweli ya wokovu wako.
(K) Kwa wingi wa fadhili zako unijibu, ee Bwana.

Shangilio

Yn 8:12

Aleluya, aleluya
Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.
Aleluya

Injili

Mt 13:54-58

Yesu alipofika nchi yake, akawafundisha katika sinagogi lao, hata wakashangaa, wakasema, Huyu amepata wapi hekima hii na miujiza hii? Huyu si mwana wa seremala? Mamaye si yeye aitwaye Mariamu? Na nduguze si Yakobo, na Yusufu, na Simoni, na Yuda? Na maumbu yake wote hawapo hapa petu? Basi huyu amepata wapi haya yote? Wakachukizwa naye. Yesu akawaambia, Nabii hakosi kupata heshima, isipokuwa katika nchi yake, na nyumbani mwake mwenyewe. Wala hakufanya miujiza mingi huko, kwa sababu ya kutokuamini kwao.

Maoni


Ingia utoe maoni