Jumanne. 26 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumamosi ya 5 ya Mwaka (Jumamosi, Februari 13, 2021)  

Somo la 1

Mwa 3:9-24

Bwana Mungu alimwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha. Akasema, Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! Umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala. Bwana Mungu akamwambia mwanamke, Nini hili ulilolifanya? Mwanamke akasema, Nyoka alinidanganya, nikala. Bwana Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako; nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino. Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala. Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako; michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula mboga za kondeni; kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi. Adamu akamwita mkewe jina lake Hawa; kwa kuwa yeye ndiye aliye mama yao wote walio hai. Bwana Mungu akawafanyia Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika. Bwana Mungu akasema, Basi, huyu mtu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya; na sasa asije akanyosha mkono wake akatwaa matunda ya mti wa uzima, akala, akaishi milele; kwa hiyo Bwana Mungu akamtoa katika bustani ya Edeni, ailime ardhi ambayo katika hiyo alitwaliwa. Basi akamfukuza huyo mtu, akaweka Makerubi, upande wa mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima.

Wimbo wa Katikati

Zab 90:2, 3-4abc, 5-6, 12-13

Kabla haijazaliwa milima, wala hujaiumba dunia,
Na tangu milele hata milele ndiwe Mungu.
(K) Wewe Bwana, umekuwa makao yetu, kikazi baada ya kizazi.

Wamrudisha mtu mavumbini, usemapo,
Rudini, enyi wanadamu.
Maana miaka elfu machoni pako Ni kama siku ya jana ikiisha kupita,
Na kama kesha la usiku.
(K) Wewe Bwana, umekuwa makao yetu, kikazi baada ya kizazi.

Wawagharikisha, huwa kama usingizi,
Asubuhi huwa kama majani yameayo.
Asubuhi yachipuka na kumea,
Jioni yakatika na kukauka.
(K) Wewe Bwana, umekuwa makao yetu, kikazi baada ya kizazi.

Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu,
Tujipatie moyo wa hekima.
Ee Bwana urudi, hata lini?
Uwahurumie watumishi wako.
(K) Wewe Bwana, umekuwa makao yetu, kikazi baada ya kizazi.

Injili

Mk 8:1-10

Katika siku zile, kwa vile ulivyokuwa mkuu tena ule mkutano, nao wamekosa kitu cha kula, akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Nawahurumia mkutano kwa sababu yapata siku tatu wamekaa nami, wala hawana kitu cha kula; nami nikiwaaga waende zao nyumbani kwao hali wanafunga, watazimia njiani; na baadhi yao wametoka mbali. Wanafunzi wake wakamjibu, Je! Ataweza wapi mtu kuwashibisha hawa mikate hapa nyikani? Akawauliza, Mnayo mikate mingapi? Wakasema, Saba, Akawaagiza mkutano waketi chini; akaitwaa ile mikate saba, akashukuru, akaimega, akawapa wanafunzi wake wawaandikie; wakawaandikia mkutano. Walikuwa na visamaki vichache; akavibarikia, akasema wawaandikie na hivyo pia. Wakala, wakashiba, wakakusanya mabaki ya vipande vya mikate makanda saba. Na watu waliokula wapata elfu nne. Akawaaga. Mara akapanda chomboni pamoja na wanafunzi wake, akaenda pande za Dalmanutha.

Maoni


Ingia utoe maoni