Jumanne. 26 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Ubatizo wa Bwana (Jumapili, Januari 10, 2021)  

Somo la 1

Isa 42:1-4,6-7

Bwana asema: Tazama mtumishi wangu nimtegemezaye; mteule wangu, ambaye nafsi yangu imependezwa naye; nimetia roho yangu juu yake; naye atawatolea mataifa hukumu. Hatalia, wala hatapaza sauti yake, wala kuifanya isikiwe katika njia kuu. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima; atatokeza hukumu kwa kweli. Hatazimia, wala hatakata tamaa, hata atakapoweka hukumu duniani; na visiwa vitaingojea sheria yake. Mimi, Bwana, nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda, na kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya mataifa; kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa gerezani waliofungwa, kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa.

Wimbo wa Katikati

Zab 29:1-4, 9-10

Mpeni Bwana, enyi wana wa Mungu,
Mpeni Bwana utukufu na nguvu;
Mpeni Bwana utukufu wa jina lake;
Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu.
(K) Bwana atawabariki watu wake kwa amani.

Sauti ya Bwana i juu ya maji;
Mungu wa utukufu alipiga radi;
Bwana yu juu ya maji mengi.
Sauti ya Bwana ina nguvu;
Sauti ya Bwana ina adhama;
(K) Bwana atawabariki watu wake kwa amani.

Sauti ya Bwana yawazalisha ayala, Na kuifichua misitu;
Na ndani ya hekalu lake Wanasema wote, Utukufu.
Bwana aliketi juu ya Gharika;
Naam, Bwana ameketi hali ya mfalme milele.
(K) Bwana atawabariki watu wake kwa amani.

Somo la 2

Mdo 10:34-38

Siku ile, Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo; bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye. Neno lile alilowapelekea wana wa Israeli akihubiri habari njema ya amani kwa Yesu Kristo (ndiye Bwana wa wote), jambo lile ninyi mmelijua, lililoenea katika Uyahudi wote likianzia Galilaya, baada ya ubatizo aliouhubiri Yohana; habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye.

Shangilio

Mk 9:7

Aleluya, aleluya
Mbingu zilifunguka na sauti ikasikilika, "Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye."
Aleluya

Injili

Mt 3:13-17

Siku ile, Yesu alirudi kutoka Galilaya mpaka Yordani kwa Yohana ili abatizwe. Lakini Yohana alitaka kumzuia, akisema, Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu? Yesu akajibu akamwambia, Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote. Basi akamkubali. Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake; na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.

Maoni


Ingia utoe maoni