Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Sikukuu ya Mt. Maria Magdalena (Ijumaa, Julai 22, 2016)  

Somo la 1

2 Kor. 5 :14-17

Upendo wa Kristo watubidisha; maana tumehukumu hivi, ya kwamba mmoja alikufa kwa ajili ya wote, basi walikufa wote; tena alikufa kwa ajili ya wote, ili walio hai wasiwe hai tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa akafufuka kwa ajili yao. Hata imekuwa, sisi tangu sasa hatumjui mtu awaye yote kwa jinsi ya mwili. Ingawa sisi tumemtambua Kristo kwa jinsi ya mwili, lakini sasa hatumtambui hivi tena, Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! yamekuwa mapya.

Wimbo wa Katikati

Zab 63: 1-5, 7-8

Ee Mungu, Mungu wangu, nitakutafuta mapema,
Nafsi yangu inakuonea kiu,
Mwili wangu wakuonea shauku,
Katika nchi kame na uchovu, isiyo na maji.
(K) Nafsi yangu inakuonea kiu, Ee Bwana.

Ndivyo nilivyokutazama katika patakatifu,
Nizione nguvu zako na utukufu wako.
Maana fadhili zako ni njema kuliko uhai;
Midomo yangu itakusifu.
(K) Nafsi yangu inakuonea kiu, Ee Bwana.

Ndivyo nitakavyokubariki maadamu ni hai;
Kwa jina lako nitaiinua mikono yangu.
Nafsi yangu itakinai kama kushiba mafuta na vinono;
Kinywa changu kitakusifu kwa midomo ya furaha.
(K) Nafsi yangu inakuonea kiu, Ee Bwana.

Maana Wewe umekuwa msaada wangu,
Na uvulini mwa mbawa zako nitashangilia.
Nafsi yangu inakuandama sana;
Mkono wako wa kuume unanitegemeza.
(K) Nafsi yangu inakuonea kiu, Ee Bwana.

Shangilio

.

Aleluya, aleluya,
Maria tuambie: sema uliyoona njiani. Kaburi lilimfadhi yule aliye Mzima; Niliona utukufu wa Kristu alipokuwa akifufuka.
Aleluya.

Injili

Yn. 20 :1-2, 11-18

Siku ya kwanza ya juma Mariamu Magdalena alikwenda kaburini alfajiri, kungali giza bado; akaliona lile jiwe limeondolewa kaburini. Basi akaenda mbio, akafika kwa Simoni Petro na kwa yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, akawaambia, wamemwondoa Bwana kaburini, wala hatujui walikomweka Lakini Mariamu alikuwa akisimama karibu na kaburi, nje yake, analia. Basi akilia hivi, aliinama na kuchungulia ndani ya kaburi. Akaona malaika wawili, wenye mavazi meupe, wameketi, mmoja kichwani na mmoja miguuni, hapo ulipolazwa mwili wake Yesu. Nao wakamwambia, Mama, unalilia nini? Akawaambia, Kwa sababu wamemwondoa Bwana wangu, wala mimi sijui walikomweka. Naye akiisha kusema hayo, akageuka nyuma, akamwona Yesu amesimama, asijue ya kuwa ni Yesu. Yesu akamwambia, Mama unalilia nini? Unamtafuta nani? Naye, huku akidhania ya kuwa ni mtunza bustani, akamwambia, Bwana, ikiwa umemchukua wewe, uniambie ulipomweka, nami nitamwondoa. Yesu akamwambia, Mariamu. Yeye akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, Raboni! (yaani, Mwalimu wangu). Yesu akamwambia. Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu. Mariamu Magdalene akaenda, akawapasha wanafunzi habari ya kwamba, Nimemwona Bwana, na ya kwamba amemwambia hayo.

Maoni


Ingia utoe maoni