Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumanne ya 16 ya Mwaka C (Jumanne, Julai 19, 2016)  

Somo la 1

Mik 7:14-15, 18-20

Walishe watu wako kwa fimbo yako, kundi la urithi wako, wakaao peke yao, mwituni katikati ya Karmeli; na walishe katika Bashani na Gileadi, kama siku za kale. Kama katika siku zile za kutoka kwako katika nchi ya Misri nitamwonyesha mambo ya ajabu. Ni nani aliye Mungu kama wewe, mwenye kusamehe uovu, na kuliachilia kosa la watu wa urithi wake waliosalia? Hashiki hasira yake milele, kwa maana yeye hufurahia rehema. Atarejea na kutuhurumia; atayakanyaga maovu yetu; nawe utazitupa dhambi zao zote katika vilindi vya bahari. Wewe utamtimilizia Yakobo kweli yako, na Ibrahimu rehema zako, ulizowaapia baba zetu tangu siku za kale.

Wimbo wa Katikati

Zab 85:1-7

Bwana, umeiridhia nchi yako, Umewarejeza mateka wa Yakobo.
Umeusamehe uovu wa watu wako, Umezisitiri hatia zao zote.
Umeiondoa ghadhabu yako yote, Umerudi na kuuacha ukali wa hasira yako.
(K) Ee Bwana, utuonyeshe rehema zako

Mungu wa wokovu wetu, uturudishe, Uikomeshe hasira uliyo nayo juu yetu.
Je! Utatufanyia hasira hata milele? Utadumisha ghadhabu kizazi hata kizazi?
(K) Ee Bwana, utuonyeshe rehema zako

Je! Hutaki kurudi na kutuhuisha, Watu wako wakufurahie?
Ee Bwana, utuonyeshe rehema zako, Utupe wokovu wako.
(K) Ee Bwana, utuonyeshe rehema zako

Shangilio

Yn 14:23

Aleluya, aleluya
Mtu akinipenda, atalishika neno langu; Na Baba yangu atampenda; Nasi tutakuja kwake.
Aleluya

Injili

Mt 12:46-50

Yesu alipokuwa katika kusema na makutano, tazama, mama yake na ndugu zake walikuwa wakisimama nje, wataka kusema naye. Mtu mmoja akamwambia, Tazama, mama yako na ndugu zako wamesimama nje, wanataka kusema nawe. Akajibu, akamwambia yule aliyempasha habari, Mama yangu ni nani? Na ndugu zangu ni akina nani? Akawanyoshea mkono wanafunzi wake, akasema, Tazama, Mama yangu na ndugu zangu! Kwa maana ye yote atakayeyafanya mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni, huyu ndiye ndugu yangu, na umbu langu, na mama yangu.

Maoni


Ingia utoe maoni