Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 16 Mwaka (Jumapili, Julai 17, 2016)  

Somo la 1

Mwa 18:1-10a

Bwana alimtokea Ibrahimu karibu na mialoni ya Mamre, alipokuwa ameketi mlangoni pa hema yake mchana wakati wa hari. Akainua macho yake akaona, na tazama, watu watatu wamesimama mbele yake. Naye alipowaona alipiga mbio kuwalaki kutoka mlangoni pa hema, akainama mpaka nchi, akasema, Bwana wangu, kama nimeona fadhili machoni pako nakuomba usinipite sasa mimi mtumwa wako. Na yaletwe basi maji kidogo mkanawe miguu, mkapumzike chini ya mti huu. Nami nitaleta chakula kidogo, mkaburudishe moyo, baadaye mwendelee, iwapo mmemjia mtumwa wenu. Wakasema, Haya, fanya kama ulivyosema. Basi Ibrahimu akaenda hima hemani kwa Sara, akasema, Himiza vipimo vitatu vya unga safi, uukande, ufanye mikate. Ibrahimu akapiga mbio kwenda kundini, akaleta ndama wa ng'ombe aliye laini, mzuri, akampa mtumishi, naye akahimiza kuiandaa. Akatwaa siagi na maziwa, na ndama aliyoiandaa, akawaandikia mbele yao, akasimama karibu nao chini ya mti, nao wakala. Wakamwambia, Yu wapi Sara mkeo? Akasema, Yumo hemani. Akamwambia, Hakika nitakurudia wakati huu huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume.

Wimbo wa Katikati

Zab 15

Bwana, ni nani atakayekaa Katika hema yako?
Ni nani atakayefanya maskani yake Katika kilima chako kitakatifu?
Ni mtu aendaye kwa ukamilifu, Na kutenda haki. Asemaye kweli kwa moyo wake,
(K) Bwana, ni nani atakayekaa katika hema yako.

Asiyesingizia kwa ulimi wake.
Wala hakumtenda mwenziwe mabaya, Wala hakumsengenya jirani yake.
Machoni pake mtu asiyefaa hudharauliwa, Bali huwaheshimu wamchao Bwana
(K) Bwana, ni nani atakayekaa katika hema yako.

Ingawa ameapa kwa hasara yake, Hayabadili maneno yake.
Hakutoa fedha yake apate kula riba, Hakutwaa rushwa amwangamize asiye na hatia.
Mtu atendaye mambo hayo Hataondoshwa milele.
(K) Bwana, ni nani atakayekaa katika hema yako.

Somo la 2

Kol 1:24-28

Nayafurahia mateso niliyo nayo kwa ajili yenu; tena nayatimiliza katika mwili wangu yale yaliyopungua ya mateso ya Kristo, kwa ajili ya mwili wake, yaani, kanisa lake; ambalo nimefanywa mhudumu wake, sawasawa na uwakili wa Mungu, niliopewa kwa faida yenu, nilitimize neno la Mungu; siri ile iliyofichwa tangu zamani zote na tangu vizazi vyote, bali sasa imefunuliwa kwa watakatifu wake; ambao Mungu alipenda kuwajulisha jinsi ulivyo utajiri wa utukufu wa siri hii katika Mataifa, nao ni Kristo ndani yenu, tumaini la utukufu ambaye sisi tunamhubiri habari zake tukimwonya kila mtu, na kumfundisha kila mtu katika hekima yote, tupate kumleta kila mtu mtimilifu katika Kristo.

Shangilio

Yn 14:23

Aleluya, aleluya
Mtu akinipenda, atalishika neno langu; Na Baba yangu atampenda; Nasi tutakuja kwake.
Aleluya

Injili

Lk 10:38-42

Ikawa katika kuenenda kwao aliingia katika kijiji kimoja; mwanamke mmoja jina lake Martha akamkaribisha nyumbani kwake. Naye alikuwa na umbu lake aitwaye Mariamu, aliyeketi miguuni pake Yesu, akasikiliza maneno yake. Lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi; akamwendea, akasema, Bwana, huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu? Basi mwambie anisaidie. Bwana akajibu akamwambia, Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi; lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa.

Maoni


Ingia utoe maoni