Masomo ya Misa
Jumamosi ya 31 ya Mwaka (Jumamosi, Novemba 07, 2020)
Flp 4:10–19
Nalifurahi sana katika Bwana, kwa kuwa sas mwisho mmehuisha tena fikira zenu kwa ajili yangu, kama vile mlivyokuwa mkinifiriri hali yangu; lakini hamkupata nafasi. Si kwamba nasema haya kwa kuwa nina mahitaji; maana nimejifunza kuwa radhi na hali yoyote niliyo nayo. Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yoyote, na katika mambo yoyote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa. Nayaweza mambo yote katika yeye atiaye nguvu. Lakini mlifanya vema, mliposhiriki nami katika dhiki yangu. Nanyi pia, ninyi wenyewe mnajua, enyi Wafilipi ya kuwa katika mwanzo wa Injili, nilipotoka Makedonia, hakuna kanisa linguine lililoshirikiana nami katika habari hii ya kutoa na kupokea, ila ninyi peke yenu. Kwa kuwa hata huko Thesalonike mliniletea msaada kwa mahitaji yangu, wala si mara moja. Si kwamba nakitamani kile kipawa bali nayatamani mazao yanayozidi kuwa mengi katika hesabu yenu. Lakini ninavyo vitu vyote na kuzidi, tena nimejaa tele; nimepokea kwa mkono wa Epafrodito vitu vile vilivyotoka kwenu, harufu ya manukato, sadaka yenye kibali, impendezayo Mungu. Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu. Sasa atukuzwe Mungu, Baba yetu, milele na milele. Amina.
Zab 112:1–5
Aleluya,
Heri mtu yule amchaye Bwana,
Apendezwaye sana na maagizo yake,
Wazao wake watakuwa hodari duniani,
Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa.
(K) Heri mtu yule amchaye Bwana.
Heri atendaye fadhili na kukopesha,
Atengenezaye mambo yake kwa haki.
Kwa maana hataondoshwa kamwe,
Mwenye haki atakumbukwa milele.
(K) Heri mtu yule amchaye Bwana.
Moyo wake umethibitika hataogopa,
Amekirimu, na kuwapa maskini,
Haki yake yakaa milele,
Pembe yake itatukuzwa kwa utukufu.
(K) Heri mtu yule amchaye Bwana.
Yn 13:13
Aleluya, aleluya,
Bwana anasema: Siwaiti tena watumwa, lakini ninyi nimewaita rafiki, kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu.
Aleluya.
Lk 16:9-15
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Jifanyieni rafiki kwa mali ya udhalimu, ili itakapokosekana wawakaribishe katika makao ya milele. Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia. Bali, kama ninyi hamkuwa waaminifu katika mali ya udhalimu, ni nani atakayewapa amana mali ya kweli? Na kama hamkuwa waaminifu katika mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewapa iliyo yenu wenyewe? Hakuna mtumishi awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana, ama atamchukia huyu au kumpenda huyu, ama atamshikamana na huyu na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali.
Maoni
Ingia utoe maoni