Masomo ya Misa
Kumbukumbu ya Mt. Karoli Boromeo, Askofu (Jumatano, Novemba 04, 2020)
Flp 2:12-18
Wapendwa wangu, kama vile mlivyotii sikuzote, si wakati mimi nilipokuwapo tu, bali sasa zaidi sana mimi nisipokuwapo, utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka. Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema. Yatendeni mambo yote pasipo manung’uniko wala mashindano, mpate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama, wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu, mkishika neno la uzima; nipate sababu ya kuona fahari katika siku ya Kristo, ya kuwa sikupiga mbio bure wala sikujitaabisha bure. Naam, hata nikimiminwa juu ya dhabihu na ibada ya imani yenu, nafurahi; tena nafurahi pamoja nanyi nyote. Nanyi vivyo hivyo furahini, tena furahini pamoja nami.
Zab 27:1,4,13-14
Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,
Nimwogope nani?
Bwana ni ngome ya uzima wangu,
Nimhofu nani?
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.
Neno moja nimelitaka kwa Bwana,
Nanlo ndilo nitakalolitafuta,
Nikae nyumbani mwa Bwana
Siku zote za maisha yangu.
Niutazame uzuri wa Bwana,
Na kutafakari hekaluni mwake.
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.
Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana
Katika nchi ya walio hai.
Umngoje Bwana, uwe hodari,
Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana.
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.
Lk 8:15
Aleluya, aleluya,
Wanabarikiwa wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao hulisikia neno la Mungu na kulishika.
Aleluya.
Lk 14:25-33
Makutano mengi walipokuwa wakifuatana na Yesu, aligeuka, akawaambia, Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume kwa wake, na wanawe, na ndugu zake waume kwa wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Mtu yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia? Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza. Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini? Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za Amani, mtu yule akali mbali. Basi, kadhlika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
Maoni
Ingia utoe maoni