Masomo ya Misa
Ijumaa ya 30 ya Mwaka (Ijumaa, Oktoba 30, 2020)
Fil 1:1-11
Paulo na Timotheo, watumwa wa Kristo Yesu, kwa watakatifu wote katika Kristo Yesu, walioko Filipi, pamoja na maaskofu na mashemasi. Neema na iwe kwenu na amani zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo. Namshukuru Mungu wangu kila niwakumbukapo, sikuzote kila niwaombeapo ninyi nyote nikisema sala zangu kwa furaha, kwa sababu ya ushirika wenu katika kuieneza Injili, tangu siku ile ya kwanza hata leo hivi. Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu; vile vile kama ilivyo wajibu wangu kufikiri haya juu yenu nyote; kwa sababu ninyi mmo moyoni mwangu; kwa kuwa katika kufungwa kwangu na katika kazi ya kutetea Injili na kuithibitisha, ninyi nyote mmeshirikiana nami neema hii. Maana Mungu ni shahidi wangu, jinsi ninavyowaonea shauku ninyi nyote katika moyo wake Kristo Yesu. Na hii ndiyo dua yangu, kwamba pendo lenu lizidi kuwa jingi sana, katika hekima na ufahamu wote; mpate kuyakubali yaliyo mema; ili mpate kuwa na mioyo safi, bila kosa, mpaka siku ya Kristo; hali mmejazwa matunda ya haki, kwa njia ya Yesu Kristo, kwa utukufu na sifa ya Mungu.
Zab 111:1-6
Aleluya, Nitamshukuru Bwana kwa moyo wangu wote,
Barazani pa wanyofu wa moyo na katika mkutano.
Matendo ya Bwana ni makuu.
Yafikiriwa sana na wapendezwao nayo.
(K) Matendo ya Bwana ni makuu.
Kazi yake ni heshima na adhama,
Na haki yake yakaa milele.
Amefanya ukumbusho wa matendo yake ya ajabu;
Bwana ni mwenye fadhili na rehema.
(K) Matendo ya Bwana ni makuu.
Amewapa wamchao chakula;
Atalikumbuka agano lake milele.
Amewajulisha watu wake uwezo wa matendo yake,
Kwa kuwapa urithi wa mataifa.
(K) Matendo ya Bwana ni makuu.
Lk 14:1-6
Yesu alipoingia ndani ya nyumba ya mtu mmoja miongoni mwa wakuu wa Mafarisayo siku ya sabato, ale chakula, walikuwa wakimvizia. Na tazama, mbele yake palikuwa na mtu mwenye ugonjwa wa safura. Yesu akajibu, akawaambia wana-sheria na Mafarisayo, Je! Ni halali kuponya siku ya sabato, ama sivyo? Wao wakanyamaza. Akamshika, akamponya, akamruhusu aende zake. Akawaambia, Ni nani miongoni mwenu, ikiwa ng'ombe wake au punda wake ametumbukia kisimani, asiyemwopoa mara hiyo siku ya sabato? Nao hawakuweza kujibu maneno haya.
Maoni
Ingia utoe maoni