Masomo ya Misa
Kumbukumbu ya Watakatifu Malaika Walinzi wetu (Ijumaa, Oktoba 02, 2020)
Ayu 38:1, 12–21, 40:3–5
Ndipo Bwana alimjibu Ayubu katika upepo wa kisulisuli, na kusema, Je! Umeiamuru asubuhi tangu siku zako zilipoanza? Umeyajulisha mapambazuko mahali pake? Yapate kuishika miisho ya nchi, waovu wakung’utwe wakawe mbali nayo? Hubadilika mfano wa udongo chini ya muhuri, vitu vyote vinatokea kama mavazi. Na waovu nuru yao huzuiliwa isiwafikie, na mkono ulioinuka huvunjika. Je! Umeziingia chemchemi za bahari, au umetembea mahali pa siri pa vilindi? Je! Umeziingia chemchemi za bahari, au umetembea mahali pa siri pa vilindi? Umeyafahamu mapana ya dunia? Haya! Sema, ikiwa unayajua hayo yote. Iko wapo njia ya kuyafikia mako ya nuru? Na giza pia, mahali pake ni wapi? Upate kuipeleka hata mpaka wake, upate kuelewa na mapito ya kuiendea nyumba yake? Hukosi unajua, maana ulizaliwa wakati huo, na hesabu ya siku za ni kubwa! Ndipo Ayubu akamjibu Mungu, na kusema, Tazama, mimi si kitu kabisa, nikujibu nini? Naweka mkono wangu kinywani pangu. Nimenena mara moja, nami sitajibu; naam, nimenena mara mbili, lakini sitaendelea zaidi.
Zab 139:1–3, 7–10, 13–14
Ee Bwana umenichunguza na kunijua.
Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu:
Umelifahamu wazo langu tokea mbali.
Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu,
Umeelewa na njia zangu zote.
(K) Uniongoze Bwana, katika njia ya milele.
Niende wapi nijiepushe na roho yako?
Niende wapi niukimbie uso wako?
Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko;
Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko.
(K) Uniongoze Bwana, katika njia ya milele.
Ningezitwaa mbawa za asubuhi,
Na kukaa pande za mwisho za bahari;
Huko nako mkono wako utaniongoza,
Na mkono wako wa kuume utanishika.
(K) Uniongoze Bwana, katika njia ya milele.
Maana Wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu,
Uliniunga tumboni mwa mama yangu.
Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa
Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha.
(K) Uniongoze Bwana, katika njia ya milele.
Yn 14:5
Aleluya, aleluya,
Bwana anasema: mimi ndimi njia, na ukweli, na uzima, mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
Aleluya.
Lk 10:13–16
Yesu aliwaambia wafuasi wake: Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza hiyo iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu tangu hapo, huku wakiketi katika nguo za kigunia na majivu. Lakini, siku ya hukumu itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zake kuliko ninyi. Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa hata mbinguni? Utashushwa hata kuzimu. Awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma.
Maoni
Ingia utoe maoni