Masomo ya Misa
Kumbukumbu ya Mt. Korneli, Papa na Shahidi (Jumatano, Septemba 16, 2020)
1Kor 12:31 13:13
Takeni sana karama zilizo kuu. Hata hivyo nawaonyesha njia iliyo bora. Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao. Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi. Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu. Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote. Upendo haupungui neno wakati wowote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma, yakiwapo maarifua, yatabatilika. Kwa maana tunafahamu kwa sehemu; na tunafanya unabii kwa sehemu; lakini ijapo ile iliyo kamili, iliyo kwa sehemu itabatilika. Nilipokuwa mtoto mchanga, nalisema kama mtoto mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri kama mtoto mchanga; tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya kitoto. Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana. Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo.
Zab 33:2-5, 12, 22
Mshukuruni Bwana kwa kinubi,
Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa.
Mwimbieni wimbo mpya,
Pigeni kwa ustadi kwa sauti ya shangwe.
(K) Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao.
Kwa kuwa neno la Bwana lina adili,
Na kazi yake yote huitenda kwa uaminfu.
Huzipenda haki na hukumu,
Nchi imejaa fadhili za Bwana.
(K) Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao.
Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao,
Watu aliowachagua kuwa urithi wake.
Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi,
Kama vile tulivyokungoja Wewe.
(K) Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao.
Efe 1:17, 18
Aleluya, aleluya,
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, awape roho ya hekima mjue tumaini la mwito wake.
Aleluya.
Lk 7:31-35
Yesu aliwaambia makutano: Niwafananishe na nini watu wa kizazi hiki? Nao wamefanana na nini? Wamefanana na watoto walioketi sokoni na kuitana, wakisema, Tuliwapigia filimbi wala hamkucheza; tuliomboleza, wala hamkulia. Kwa kuwa Yohane Mbatizaji alikuja, hali mkate wala hanywi divai, nanyi mwasema, Ana pepo. Mwana wa Adamu amekuja, anakula na kunywa; nanyi mwasema, Tazama, mlafi huyu, na mnywaji wa divai, rafiki wao watoza ushuru na wenye dhambi. Na hekima imejulikana huwa ina haki kwa watoto wake wote.
Maoni
edwin msekalile
NENO LA BWANAA!Ingia utoe maoni